0
 
 MKUU WA WILAYA YA BUTIAMA AKIWA KATIKA PICHA NA WANAFUNZI WA KIKE WA SHULE MBALIMBALI WILAYANI HUMO BAADA YA KONGAMANO
 
WANAFUNZI  wa  kike  2,425  katika shule  mbalimbali  za  Sekondari  wilaya ya Butiama  mkoani Mara, wameshindwa kuendelea  na  masomo yao  ya Sekondari kutokana na  sababu  mbalimbali  ikiwemo  ya  kupata mimba  na  kulazimishwa kuolewa  na wazazi  wao.
 
Mkuu wa wilaya ya Butiama Angelina Mabula,ametoa taarifa hiyo  katika kongamano la  kujadili  hali  ya  elimu  kwa watoto wa kike wilayani humo, huku akisema  wanafunzi hao ni kati  ya 7,818  walijiunga na kidato  cha  kwanza katika kipindi  cha  miaka mitatu.
 
 
Amesema idadi hiyo ni kubwa na inarudisha nyuma maendeleo ya elimu kwa mtoto wa kike hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu lazima kuhakikisha inapambana na hali hiyo.
 
Mabula ameeleza kuwa suala la elimu haliwezi kuachwa nakuona wanafunzi wa kike wakipata mimba na kuozwa na wazazi na kutaka kila mmoja kutoa taarifa anapoona jambo hilo hili yoyote anayehusika na kukwamisha maendeleo ya elimu aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
 
Mkuu huyo wa Wilaya amesema katika siku za hivi  karibuni  imebainika  tena  kuna wanafunzi  wengine  wa  kike  zaidi  ya  40   wamegundulika kuwa na  ujauzito katika halmashauri ya Butiama wakati uchunguzi ukiendelea katika halmashauri ya Musoma.
 
Kwa upande wake mgeni rasmi katika kongamano hilo,Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake  Tanzania (UWT) Amina Makilagi,pamoja na kusikitishwa na ukubwa wa tatizo  la  vikwazo  vya  elimu  kwa  mtoto  wa  kike  wilayani Butiama,amewataka wanafunzi hao  wa kike  kutoka shule mbalimbali   za  sekondari  wilayani humo,kuepukana  na  vishawishi ambavyo   alisema vinaweza  kukatisha  ndoto  zao  katika maisha.
 
Amesema lazima mtoto wa kike asome aweze kukabiliana na changamoto mbalibali za maisha na kila mmoja asikubali kuona motto wa kike akiishia kupata mimba na kuozwa akiwa anasoma.
 
Makilagi amewataka watoto wa kike kujitambua na kulipa kipaumbele suala la elimu kama nguzo kuu ya maisha na pale wanapoona mtu yoyote anataka kumuharibia msingi wa maisha kumtolea taarifa kwenye vyombo vya dola.

Post a Comment