0
 
Mabingwa wa muziki wa dansi nchini Msondo Ngoma na  Mlimani Park Orchestra “Sikinde” kesho  mchana zitachuana vikali katika viwanja vya TCC Club  Chang’ombe, Temeke.
Mpambano huo wa kusherekea sikukuu ya Krismasi litakuwa la kufunga mwaka 2013 na pia litaamua ni bendi gani bora kati ya magwiji hao wa muziki wa dansi nchini mwaka huu.
Mratibu wa mchuano huo Joseph Kapinga amesema pambano huo litanzaza saa nane alasiri hadi majogoo.
Kapinga alisema Sikinde wataingia TCC wakitokea Bagamoyo walipokuwa wakipiga kambi wakati kambi ya Msondo Ngoma imebaki kuwa siri kwa muda wote.
Mratibu huyo alisema kila bendi litapiga kwenye jukwaa lake ili kuondoa hujuma.Kapinga alisema kila bendi itatapewa muda wa saa moja kupiga jukwaani kabla ya kumpisha nyingine.
Kiongozi wa Msondo Ngoma Saidi Mabera  alisema jana kuwa watapiga nyimbo zao zote kali ili kuhakikisha wanaibuka kidedea.
Alitaja baadhi ya nyimbo ambazo watazipiga kuwa ni  'Nimuokoe Nani', 'Zarina', 'Mwanaidi', 'Kanjelenjele', 'Bahati', 'Sesilia', 'Usiue Usiibe', 'Asha Mwana Seif', 'Kauka Nikuvae', Chuma Chikoli Moto', 'Kilio cha Mzima', 'Ajali' na  'Suluhu'.
Baadhi ya wanamuziki wanaounda Msondo Ngoma ni Shaaban Dede, Mabera, Abdul Ridhiwani Pangamawe, Athumani Kambi, Saad Ally 'Mashine', Eddo Sanga, Huruka Uvuruge, Zahoro Bangwe, Ibrahim Kandaya,  James Mawilla,  Juma Katundu, Hamisi Mnyupe, Roman Mng’ande `Romario’  na Hassan Moshi.
Naye kiongozi wa Sikinde Hamisi Mirambo alijigamba kuwa wataibuka na ushindi mnono.“Tuna waimbaji wazuri na hakuna itakachotuzuia kushinda,” alisema Mirambo.
Alitaja baadhi ya nyimbo ambazo watazipiga kuwa ni 'Selina', Wiki endi', 'Penzi la Fukara', 'Hiba', 'MV Mapenzi’,  'Supu Umelitia Nazi' na 'Jinamizi la Talaka'.
Sikinde inaundwa na wanamuziki kama Hassan Rehani Bitchuka, Hassan Kunyata, Kaingilila Maufi, Tonny Karama, Shaaban Mabuyu, Habib Abassi, Juma Choka, Ally Jamwaka,  Mbaraka Othman, Hamisi Milambo, Shaaban Lendi, Joseph Benard, Ramadhani Mapesa na Habibu Jeff.
Pambano umeandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts chini ya udhamini wa Konyagi, Nipashe, CXC Africa na Saluti5.

Post a Comment