0
  -Wananchi walaumu Polisi kwa uzembe

      Na Shomari Binda
           Musoma,


Watu 13 wamefariki Dunia na wengine 14 kujeruhiwa kutokana na ajali ya gari iliyotokea jana (juzi)jioni katika Kijiji cha Mkiringo Wilaya ya Butiama Mkoani Mara ikiwa safarini kutoka Musoma Kuelekea Nyamswa-Butiama.

Mashuhuda wa ajali hiyo iliyohusisha gari aina ya Toyota Hiace lenye namba T123 CAE iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Joseph maarufu kama Diouf ilikuwa katika mwendo kasi huku ikiwa imebeba abiria kupita kiasi waliokuwa katika safari hiyo.

Wameeleza gari hilo likiwa katika mwendo huo wa kasi lilipasuka tairi la nyuma upande wa kulia na kupinduka mara tatu na kupelekea vifo pamoja na majeruhi hao waliolazwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.

Mganga mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mara docta Samsoni Wenani aliwaeleza Waandishi wa Habari waliofika Hospitalini hapo amepokea majeruhi pamoja na maiti waliohifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali hiyo.

Docta Wenani aliwataja maiti 12 ambao walitambuliwa na ndugu zao huku mmoja akiwa bado hajatambuliwa kuwa ni dereva wa gari hilo Emmanuel Joseph,Pendo John (39) pamoja na mtoto wake Joseph Richard (5) wakazi wa Bisarye,Razak Shaabani,Hamis Kanyoro,Nyamazore John,Innocent Fares Kweka na Jiadhari Saidi Dogori wakazi wa Nyamswa.

Wengine waliotajwa kufariki katika ajali hiyo ni Aizaki Hassan,Makuli Maguri pamoja na watu wengine wawili waliotambulika kwa jina moja moja la Masoke na Richard ambao ni wakazi wa Wilayani Butiama.

Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Mkoa wa Mara aliwataja majeruhi katika ajali hiyo wanaoendelea na matibabu huku hali zao zikiendelea vizuri kuwa ni Nyamakunguru Fanuel,Nyamazege Warioba,Gosbert Waryoba,Hamisi Wisaka,Hamisi Gibombi na Hamis Nyaga.

Watu wengine waliojeruhiwa katika ajali hiyo na kulazwa katika Hospitali hiyo ni pamoja na Mganda Nyamajege,Efrancia Kiamanzi pamoja na Beatrice Siriwa ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chief Ihunyo waliokuwa wakitokea Jijini Dar es salaam kuelekea shuleni.

Majeruhi wengine ni pamoja na Mwalimu wa shule ya msingi Butiama B Betrece Komba ambaye amevunjika sehemu ya juu ya mguu wake wa kulia,Bunuli Madube pamoja na mtoto wa miaka 8 Matha Makuli ambaye baba yake waliyekuwa naye katika ajali hiyo alifariki Dunia.

                        WANANCHI WALAUMU JESHI LA POLISI

Kutokana na kutokea kwa ajali hiyo iliyopelekea vifo vya watu 13 na majeruhi 14 Wananchi Mkoani Mara wamelahumu Jeshi la Polisi Mkoani Mara kwa kushindwa kusimamia ujazo wa abiria katika gari kabla ya kuanza kwa safari na kupelekea vifo ambazo vinaweza kuzuilika.

Mmmoja wa Wananchi katika Stendi ya Nyasho aliiambia blogu hii kuwa gari hilo alilishuhudia likianza safari ya kuelekea Butiama huku likiwa limejaza kupita kiasi huku Jeshi la Polisi likishindwa kuchukua hatua yeyote.

"Mimi nililishuhudia gario hilo kwa macho yangu likianza safari na lilikuwa limejaza sana huku sehemu ya mbele ya abiria ambapo kimsingi hukaa watu wawili walikuwa wamekaa wanne"alisema Mwananchi huyo ambaye hakupenda kutaja jina lake.

Alisema haoni kazi inayofanywa na askari wa usalama barabarani ikiwa wanashindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo na lawama zote za ajali hiyo zinapaswa kupelekwa kwao kwa kuwa wao ndio wasimamizi wa usalama barabarani.

Post a Comment