0
 CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI MARA CHALAANI MAUAJI YA MWANDISHI
     Na Shomari Binda 
           Musoma 

Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Mara (MRPC) kimelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa na kupelekea kifo cha Mwaandishi wa Habari wa Chanel ten na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Iringa (IPC) Daudi Mwangosi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya maadili kwa Waandishi wa Habari yanayotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mara katika ukumbi wa Orange Tree,Mwenyekiti wa (MRPC) Emanuel Bwimbo amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwandishi huyo.

Amesema nguvu kubwa inayotumiwa na Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yao na kusababisha maafa katika jamii hakipaswi kukaliwa kimya na kuona vitendo vya namana hiyo vikiendelea kutokea katika jamii.

Bwimbo amesema ni vyema kwa askari wa Jeshi la Polisi kijifunza mbinu mbadala katika kutekeleza majukumu yao ili kuweza kuepusha maafa ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kupitia kwao.

Amesema haiwezekani kwa kipindi cha muda mchache askari Polisi kudaiwa kusababisha ya watu wanaozidi watatu katika mnaeneo mbalimbali hapa Nchini kutoikana na matumizi ya nguvu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ameeleza Mwandishi wa Hbari Daudi Mwangosi ameuwawa akiwa anatekeleza majukumu yake na kuongeza kuwa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Mara kinaendelea kulaani tukio hilo.

Kwa upande wake Mwandishi wa Habari Mwandamizi na Mwanasheria wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Mara Juma Thomas amesema amesikitishwa na kifo cha Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi na matumizi ya nguvu ya Jeshi la Polisi.

Amesema Sheria inaeleza Polisi kutokutumia nguvu kubwa katika kutekeleza majukumu yao na walipaswa kumlinda Mwandishi  huyo asipate matatizo katika kufanya kazi yake ya ukusanyaji na upashaji wa Habari.
 
Tayari Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeunda Tume Huru  kwenda Mkoani Iringa kuchunguza kifo cha Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi

Post a Comment