0
Wanafunzi wawili wa darasa la sita katika shule ya msingi nyamwaga iliyopo katika kijiji cha Nyakunguru  kata ya Kibasuka Wilayani Tarime wamefariki dunia baada ya kuzama katika dimbwi la maji na kushindwa kuogelea na kupoteza maisha.

Akizungumza na BLOG HII ofisini kwake,Kamanda wa polisi kanda maalum Tarime na Rorya Justus Kamugisha alisema wanafunzi hao waliofahamika kwa majina ya Richard Mniko (16) na Mniko Melengali (16) walizama aprili 28 katika dimbwi hilo wakiwa wanaogelea na kuzidiwa na maji yaliyoko katika dimbwi hilo.

Kamanda Kamugisha alisema dimbwi hilo lilitokana na kuchimbwa kwa kifusi kwa ajili ya kutengeneza barabara ya mpya kutoka Nyamwaga kwenda Serengeti na limejaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Wilayani Tarime.

Kufuatia tukio hilo kamanda Kamugisha amewaomba wazazi ambao wapo karibu na dimbwi hilo kuwa makini kwa kuwaangalia watoto ili wasiweze kucheza karibu na eneo hilo na sehemu nyingine ambapo maji yametuama kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha.

Katika tukio lingine Kamugisha alisema jeshi la polisi kanda maalum Tarime na Rorya linaendelea kufanya uchunguzi kutokana na tukio la mauaji ya Mwikwabe Wankuru Marwa (25) aliyuwawana kitu chenye ncha kali aprili 28 na watu zaidi ya wanne waliotambuliwa kwa majina na sura.

Alisema tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Nyakunguru ambapo marehemu alichomwa mgongoni,kichwani na kwenye mkono wa kulia ambapo kamanda Kamugisha alidai chanzo cha mauaji hayo ni watuhumiwa kutaka kumnyang'anya panga ndugu wa marehemu huku watuhumiwa hao wakitoroka baada ya kutenda kosa hilo.

Kamanda Kamugisha ameendelea kutoa wito kwa Wananchi wa Tarime kutii sheria na kuacha kujichukulia sheria mkononi na kusababisha vifo ambavyo vinaendelea kupunguza nguvu kazi katika Taifa na kusababisha chuki ambazo zinaweza kuongeza matukio ya mauaji.

Post a Comment