1











WAGANGA pamoja na jamii ya Watanzania imeaswa kujijengea tabia ya kuhifadhi miti na mimea inayotoa tiba asilia kwa kujianzishia bustani na misitu maalum ili kujihakikishia maliasili hiyo haipoteii kutokana na umuhimu wake.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Afya Mwandamizi wa hospitali teule ya Nyerere DDH ya Mugumu Wilayani Serengeti Dr.Musoto Chirangi katika hafla fupi ya mapokezi yake baada ya kuhitimu shahada ya uzamivu wa  afya ya jamii katika chuo kikuu cha  Leiden cha Nchini Uholanzi.   

Alisema waganga na wataalamu wa miti shamba inayotibu kama hawatatilia maanani kuuratibu utaalamu wao na kuuhifadhi katika vitabu kama inavyofanyika katika Nchi mbalimbali duniani zikiwemo China,Malasia na Indonesia tiba asilia itapotea kabisa.

"Wapo watu ambao wana utaalamu wa kutibu na kuponya kutumia tiba asilia lakini hakuna kumbukumbu yoyote nzuri ambayo wanaiacha kwa kuandika walau kitabu juu ya tiba aliyoitoa kupitia mizizi,magamba ama matawi sasa kwa hali hii mtaalamu wa tiba asilia anapofariki basi na tiba yake inakufa.

"Kuna kila sababu ya kuhifadhi mimea tiba na kujianzishia bustani za maliasili hiyo ili kuendelea kupata matibabu kwa kutumia tiba asilia na hili sio la kuwaachia watu wachache maana umuhimu wa jambo hili unafahamika,"alisema Musoto.

Alisema dunia ya sasa kila mahala wamekuwa wakizipa umuhimu dawa za tiba asilia na kuendelea kufanya tafiti mbalimbali ya tiba hiyo ili kuweza kuisaidia jamii katika masuala ya tiba na kudai kuna kila sababu kwa Nchi ya Tanzania kuona namna ambayo itashirikiana na wataalamu hao.

Alidai katika tafiti yake juu ya tiba asilia pamoja na tiba ya kitaalamu aliyoiweka kwenye kitabu cha kurasa 301 na maneno 127,335 ameona bado kuna changamoto Nchini Tanzania ambapo wataalamu wa tiba asilia wamekuwa hawapewi nafasi ya kutosha kuelezea tiba zao wanazozitoa na wengine ufikia kuiaga dunia bila kuacha maandiko yoyote katika kizazi wanachokiacha.

Aliongeza kuwa China inawatumia sana wataalamu wa tiba asilia na kuwasaidia katika tafiti zao wanazozifanya hali ambayo imepelekea leo nchi hiyo asilimia kubwa ya madawa wanayotumia yanatokana na tiba asilia na mengine kuletwa hapa nchini huku yakiuzwa kwa watanzania kwa bei ya juu.

 Aidha dokta Musuto aliwataka wasomi hapa Nchni kuutumia usomi walioupata katika kuwasaidia watanzania katika masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia masuala muhimu ambayo yanaigusa jamii. 

Post a Comment

Hongera zake kufikia hatua hiyo ya juu kielimu. Binda mimi nimefurahishwa na msisitizo wa umuhimu wa kufanya tafiti na kutumia matokeo yake.