0
WATU wawili wakazi wa Nyamaguku wilayani Rorya na Nyamatare katika Manispaa ya Musoma wamekutwa wamekufa kwa kujinyonga mmoja kwa kutumia shati na fulana ya ndani na mwingine kwa kutumia kamba ya katani kwa nyakati tofauti.

Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake,Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Mara Kamishina Msaidizi Paul Kasabago, amesema katika tukio la kwanza mnamo juni 24 majira ya saa 3 usiku, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Paschal Mwamba Lukonge (45) Mkazi wa Nyamatare katika Manispaa ya Musoma alikutwa amejinyonga katika chumba chake kwa kutumia kamba ya katani.

Amesema katika tukio hilo mtu huyo kabla ya kujinyonga,juni 23 majira ya jioni alizozana na mama yake mzazi aitwaye Chausiku Maguri (79) baada ya kumuuliza marehemu pesa za mauzo ya sigara alizokabidhiwa auze kwenye klabu ya pombe za kienyeji aina ya wanzuki,na kutokana na mzozo huo marehemu alitishia kujiua.

Kasabago amesema baada ya kuzozaana marehemu alikwenda kulala katika chumba ambacho analala peke yake ndipo asubuhi majira ya saa 2 alipogunduliwa tayari amejinyonga.

 Tukio la pili amesema mnamo juni 25 majira ya saa 11 jioni katika Kijiji cha Mangoro Wilaya ya Butiama,mtu mmoja aitwaye Chacha Nchura Mkazi wa Nyamaguku wilayani Rorya alikutwa amejinyonga kwa kutumia shati lake na fulana ya ndani huku mwili wake ukiwa umening'inia juu ya mti.

Kaimu kamanda huyo alisema uchunguzi wa matukio hayo ya kujinyonga bado unaendelea huku akitoa wito kwa Wananchi kutafuta njia ya kutatua matatizo kuliko kuchukua maamuzi ya kujinyonga.

Katika tukio lingine la kushangaza,Mtoto mwenye umri kati ya mwezi mmoja na miezi 9 amekutwa hana pua na mdomo sehemu ya juu baada ya kufariki dunia akiwa anapata matibabu kwa mganga wa kienyeji.

Akielezea tukio hilo,Kasabago amesema lilitokea katika maeneo ya Nyasura Kata ya Nyasura wilayani Bunda baada ya wazazi wa mtoto huyo kumfikisha nyumbani baada ya kufariki na kumkuta akiwa hana viungo hivyo.

Amesema mtoto huyo akiwa anaendelea kutibiwa kwa mganga wa kienyeji,juni 23 alifariki dunia na juni 24 majira ya asubuhi wakiwa nyumbani iligundulika hana viungo hivyo huku akidai uchunguzi wa tukio hilo unafanywa ili kubaini sababu zilizopelekea mtoto huyo kuondolewa viungo huku kukiwa hakuna mtu yoyote aliyekamatwa kutokana na tukio hilo








Post a Comment