0

SHIRIKA la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) limetoa msaada wa mabati elfu sita yenye thamani ya shilingi milioni 124 kwa ajili ya kuezekea vyumba vya madarasa,nyumba za walimu,vituo vya afya pamoja na vituo vya polisi katika Wilaya ya Tarime.

Akipokea msaada huo katika viwanja  vya sabasaba Mjini hapa,Mkuu wa mkoa wa Mara Gabriel Tupa alisema msaada huo umekuja wakati muafaka kukiwa na changamoto za kumalizia baadhi ya vyumba vya madarasa pamoja na nyumba za walimu ambavyo vilikuwa havijakamilka.

Alisema msaada huo uliotolewa na Tanapa kila kiongozi anatakiwa kutimiza wajibu wake kwa kuusimamia vizuri kuhakikisha lengo la kutolewa kwake linakamilika kwa kuezeka vyumba vilivyokusudiwa kwa wakati muafaka na kuacha kuyatunza mabati hayo.

"Viongozi wenzangu kila mtu kwa nafasi yake,tuhakikishe msaada huu unafanya kazi iliyokusudiwa kwa kwenda kuezeka vyumba vya madarasa,nyumba za walimu,vituo vya afya pamoja na vituo vya polisi kwa wakati.

"Tanapa wameona umuhimu wa elimu kwa vijana wetu,afya pamoja na suala la ulinzi katika jamii,mabati haya yaliyotolewa yasibadilike matumizi yake nami ntakuwa mstari wa mbele kufatilia kwa kipindi cha muda mfupi kuona utekelezaji wake.

Akizungumzia suala la ujangiri katika hifadhi,Mku wa mkoa wa Mara alisema Wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa Tanapa kuhakikisha vitendo vyote vya ujangiri katika hifadhi vinakomeshwa kwa kutoa taarifa pale wanapoona vitendo vya ujangiri hifadhini.

Alisema misaada ya kijamii ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na Tanapa inatokana na utalii unaofanywa katika hifadhi hivyo kufanyika kwa vitendo vya ujangiri kutapelekea kupunguza utalii na hivyo kuikosesha Tanapa mapato.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa wa Mara aliwataka Wananchi kutokuingilia maeneo ya hifadhi na kusababisha migogoro isiyo ya lazima baina ya Wananchi na askari wanyamapori ambayo imekuwa ikitokea katika baadhi ya maeneo ya hifadhi.

Alisema katika suala la kuingilia maeneo ya hifadhi wanasiasa pia wamekuwa wakichangia kwa kutokuwaeleza Wananchi ukweli juu ya sheria za hifadhi na kupelekea kuvamia maeneo hayo na kusababisha migogoro na kuwataka kuacha kufanya hivyo.

Awali akizungumza katika makabidhiano hayo,Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa Alan Kijazi alisema Wananchi wa Kata za Nyanungu,Gorong'a na Nyarukoba ambazo zinaingia eneo la hifadhi ya Serengeti kushirikina na Tanapa katika uhifadhi wa mazingira na kutunza hifadhi.

Alisema licha ya kushugulika na uhifadhi Tanapa inalo jukumu la kushiriki katika shughuli za kijamii na msaada walioutoa sio mwisho wa ushiriki shughuli hizo.





Post a Comment