0
 
MTU mmoja aliyemtapeli Mkuu wa mkoa wa Mara na Maafisa wa Usalama mkoani hapa amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu baada ya kujitambulisha kuwa yeye ni Afisa Usalama kutoka Makao Makuu anahitaji Ulinzi wa Usalama dhidi yake ili kufikia adhima yake ya kutambua uuzaji wa risasi na bunduki kutoka Kikosi cha Jeshi cha 27KJ mkoani hapa.
 
Awali akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Musoma  Richard Maganga alisema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ulidai  Juni  17 mwaka huu mtuhumiwa aliyemtaja kwa jina la Liso Chacha alimpigia simu Mkuu wa mkoa John Tupa kuwa yeye ni Afisa Usalama toka Makao Makuu aliyeagizwa kuja mkoani Mara kwa lengo la kufuatilia mtandao wa kuuza risasi na bunduki kutoka katika kikosi cha jeshi 27 KJ kilichopo Makoko.
 
Hakimu Maganga alisema  baada ya RC kupata taarifa hizo alimpigia simu Mkuu wa Kikosi cha Jeshi cha Makoko akimtaka kuwasiliana na mtuhumiwa huyo kwa lengo la kufanikisha shughuli iliyomleta Afisa huyo tapeli.
 
Maganga alisema katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo wa watu saba wa upande wa mashitaka ulikuwa ukimtuhumu mshitakiwa kuwa alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ni Afisa wa Usalama kutoka Makoa Makuu na kuwataka wampe ushirikiano katika kufuatili mtandao wa wizi wa risasi na bunduki uliokithiri mkoani Mara.
 
Alisema mshitakiwa huyo alipokelewa na Afisa wa Jeshi na kumpa malazi katika nyumba ya mapumziko ya jeshi na kumgharamikia chakula na huduma zingine muhimu ikidhaniwa ni Ofisa wa Usalama wa Taifa kama alivyojieleza.
 
Hakimu Maganga aliendelea kusema siku iliyofuata Afisa huyo wa Jeshi alimfuata Afisa wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasi(FFU) kwa lengo la kumsaidia kumpa ulizi wa kumsindikiza mtuhumiwa huyo kufanya upekuzi kwa baadhi ya magari aliyowatajia kuwa yatapita katika beria ya polisi iliyopo eneo la Kirumi.
 
Afisa huyo pia alimpatia askari wawili ambao waliambatana nao katika eneo hilo na kuanza kukagua magari kwa muda wa siku mbili bila kufanikisha kitu chochote,hivyo wakawa wamejipanga kurudi tena kwa siku ya tatu.
 
Hakimu alisema kabla hawajaondoka siku hiyo ya tatu mtuhumiwa huyo aliingia katika Ofisi ya wanahabari kwa lengo la kutaka msaada kutoka kwao lakini mahojiano na wanahabari hao walimshutukia na kutoa taarifa kwa Afisa Usalama wa mkoa na maeneo mengine hali iliyopelekea kumtia hatiani kwa wakati ule.
 
Kwa upande wa Idara ya Usalama wa Taifa Makao Makuu walipoulizwa kuhusiana na tuhuma za mtuhumiwa huyo walidai hawajamtuma mtu kufanya shughuli ya aina hiyo mkoani hapa na kwamba katika orodha ya watumishi wa Usalama wa Taifa hapa nchini hakuna jina kama hilo,ilieleza sehemu ya Hukumu hiyo.
 
Hakimu alisema ni kinyume cha Sheria na taratibu mtu kujitambulisha  kwa nafasi isiyo yake na kwamba mshitakiwa anahitaji adhabu kali na adhabu kubwa kulingana na kosa hilo alilofanya ni kutumikia jela miaka mitano,lakini kufuatia maombi ya mtuhumiwa kuwa anao watoto wanaomtegemea atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
 
Mwendesha mashitaka wa jeshi la polisi Stephano Mgaya aliiambia Mahakama kuwa mtuhumiwa alifanya kosa la jinai kuidanganya Serikali na kuchafua vyombo vya dola kuwa ni mtumishi wa umma na pia ameagizwa na idara ya Usalama Makao Makuu kufanya uchunguzi wa mtandao wa wizi wa silaa jambo ambalo ni uongo.
 
Mgaya alisema mtuhumiwa anastahili adhabu kali kwa kuipaka Serikali matope ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia ya kufanya udanganyifu wa kujipa nyadhifa ambazo sio zao na kufanya utapeli.
 
Baada ya Hukumu ya kufungwa miaka mitatu mtuhumiwa huyo,baadhi ya wananchi waliokuwa nje ya Mahakama kwa lengo la kusikiliza hukumu hiyo walidai uongozi wa Usalama mkoani hapa hauna maana kama mtu wa kawaida ananweza kuwaeleza jambo na wakamfuata bila hata kumuhoji ni hatari kubwa.

"Haiwezekani kwa muda wa siku tatu maafisa wa Usalama wa JWTZ NA Polisi kushindwa kumtambua mtu huyo na kumpa hifadhi zote katika makazi ya maafisa wa jeshi hadi Waandishi wa Habari wamshuku ndio hakamatwe hii ni hatari kubwa ya kiusalama.
 
“Ningekuwa mimi ndio Hakimu huyu jamaa ningemfunga siku moja tu,manake wenye kutambua kuwa huyu ni mdanganyifu ni viongozi wa usalama wa mkoani hapa,kwa kuanzia kwa mkuu wa mkoa”alisema Daniel Nyasaungu.

Post a Comment