0
 KAMANDA MTUI


KAMANDA wa jeshi la polisi mkoani Mara Ferdinand Mtui ametoa onyo kali kwa mtu yoyote atakayesherehekea mwaka mpya kwa kuchoma moto ama kupiga mafataki usiku wa leo ataishia mikononi mwa jeshi la polisi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake,Kamanda Mtui amesema jeshi la polisi limejipanga vizuri kuhakikisha wale wote watakaoenda kinyume na maelekezo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Amesema kuchoma moto barabarani ni kosa la jinai kama yalivyo makosa mengine na kuwataka wananchi kuukaribisha mwaka mpya kwa amani na utulivu ili kuepuka kuishia mikononi mwa polisi.

Kamanda huyo wa jeshi la polisi mkoani Mara amesema askari wake wamejipanga vizuri kukabiliana na mtu ama watu watakaotaka kuutumia mwanya wa sherehe za mwaka mpya kufanya uhalifu na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Ameongeza kuwa ili kuona namna walivyojipanga doria kali litaanza saa tisa mchana katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mara na kudai yoyote aliyepanga kutaka kufanya uhalifu aache maana ataishia mikononi mwa polisi.

Katika hatua nyingine,kamanda Mtui amesema kuwa katika kuendelea na oparesheni mbalimbali,jeshi hilo limefanikiwa kupataa bunduki aina ya SMG.NO.UC 5677-1998 ikiwa na magazine yenye risasi 12 iliyosalimishwa jirani na kituo kidogo cha polisi Isenye Wilayani Serengeti.

Amesema jeshi la polisi linaendelea na msako mkali wa kumtafuta mmiliki wa bunduki hiyo ambayo imedaiwa kutumika katika matukio mbalimbali ya kiuhalifu huku akitoa wito kwa wananchi wanaomiliki siraha kinyume cha sheria wazisalimishe mara moja polisi au kwa viongozi wa Serikali wanapoishi.

Post a Comment