0

MCHUNGAJI wa Kanisa la  Apostolic lililoko  mji mdogo wa Shirati
wilayani Rorya  mkoa wa Mara ameuwawa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kwa kupigwa risasi katika tukio lilotokea usiku wa
kuamkia leo (jana).

Hata hivyo Kamanda wa jeshi la polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya
Justus Kamugisha licha ya kukiri kutokea kwa tukio hilo alisema hajui
kama aliyeuwawa ni mchungaji na kwamba jeshi hilo linaendelea na
uchunguzi.

Habari zilizopatikana kutoka katika eneo la tukio zimemtaja mchungaji
huyo kuwa ni Owiti Ariri na kwamba aliuwawa muda mchache baada ya
kukabidhiwa sanduku la fedha za kikundi chao cha kuweka na kukopa
alichokuwa akikifanyia kama mhazini wake.

Kwa mujibu wa habari hizo zilizothibitishwa na mchungaji mwenzake
aitwaye Christopher Nyaitega,mara baada ya tukio hilo lililofanyika
majira ya alasiri katika moja ya hoteli iliyoko katika mji
huo,Marehemu huyo alielekea nyumbani  kwake akiwa na sanduku hilo
lililokuwa limejaa fedha.

Mchungaji Nyaitega ambaye hata hivyo hakuweza kujua kiasi cha fedha
kilichokuwemo ndani ya sanduku hilo kwa kuwa yeye siyo mmoja wa
wanakikundi,alisema wanakikundi waliamua kumkabidhi fedha hizo ili
aziwashilishe benki kesho yake.

Alisema akiwa nyumbani kwake alifikiwa na mmoja
wanakikundi wenzake aliyeanza kudadisi kuhusu fedha hizo ambapo
marehemu alimhakikishia kuwa ziko salama hali iliyomfanya mgeni wake
huyo aondoke.

Mchungaji Nyaitega alisema masaa machache tangu mgeni huyo aondoke
ghafla majambazi walifika nyumbani hapo na kumtaka marehemu awape
fedha hizo kabla ya kumuua kwa kumpiga risasi baada ya kuwa wametimiza
azma yao ya kuondoka na kiashi hicho cha fedha.

Kamanda Kamugisha alisema jeshi hilo linamshikilia mwanakikundi huyo
kwa mahojiano zaidi huku akiahidi kutoa taarifa zaidi kuhusiana na
idadi kamili ya fedha zilizochukuliwa na majambazi hao.

Post a Comment