0
 MBUNGE wa Jimbo la Musoma mjini,Vedastus Mathayo,amekamilisha ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 200 kwaajili ya kuwasaidia wanawake katika shughuli za ujasiliamali.

Wakati wa kampeni hizo za uchaguzi,Mathayo,aliyekuwa akigombea nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM),aliahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 200 kwaajili ya kuwasaidia wanawake na milioni 50 za kuwawezesha vijana kiuchumi.

Akizungumza na wenyeviti wa mitaa 73 ya Jimbo la Musoma mjini watakao husika kusajili vikundi vya wanawake watakaowezeshwa fedha hizo,Mbunge huyo alisema mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi sasa ni utekelezaji wa ahadi zilizoahidiwa ili kuwasaidia wananchi.

Alisema alipokuwa akitoa ahadi hiyo ilikuwa sio kutafuta kura pekee bali alikuwa na dhamira ya kuwataka kuwasaidia wananchi kupitia shughuli zao za ujasilimali ili waweze kuwa na uchumi bora na kuondokana na umasiki.

Mathayo alisema ametoa fedha hizo na ahitaji kurudishiwa bali ziwe na mpango mzuri ambao utaweza kuwawezesha wananchi kuzitumia kwa lengo la kuongeza kipato kwa kufanya ujasiliamali na sio kuzitumia kwa njia isiyofaa.

"Nimetoa fedha hizi kama ruzuku katika kuwasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Musoma mjini,niliahidi na nimetekeleza na kinachohitajika ni usimamizi kuona fedha hizi zinatumika kuwasaidia.

"Nawaomba wenyeviti msaidie kusajili vikundi vya watu watano ambao mtawasajili kwa kuwa nyie ndio mnawafahamu na mtashirikiana na watu walioteuliwa kufanya zoezi la utoaji wa fedha ili zinapotolewa ziende zikafanye kazi za kujenga uchumi,"alisema Mathayo.

Kuhusu utaratibu mzuri wa kusimamia fedha hizo,Mbunge huyo alisema amekubaliana na uongozi wa Imara saccos iliyopo Musoma kwa kushirikiana na watu wawili aliyewateua kuweza kuweka mipango mizuri ambayo itaweza kuwasimamia wananchi kuzitumia fedha hizo kwa kuinua kiwango cha maisha.

Mwenyekiti wa Imara saccos,Boniphace Ndengo,alisema wamepewa dhamana ya kusimamia fedha hizo na watahakikisha wanatoa elimu ya ujasilimali kwa wananchi kabla ya kuwakabidhi fedha ili ziweze kuwasaidia kwa kujiongezea kipato.

Alisema utaratibu umewekwa vizuri na rahisi za upatikanaji wa fedha hizo kupitia wenyeviti wa mitaa na kuwataka wanawake wanaolengwa na fedha hizo kufika kwenye ofisi za serikali za mitaa na kuanza taratibu za kujiunga kwenye vikundi.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

 

 









Post a Comment