0


Na Shamari Binda,Tarime

ZAIDI ya malori 30 yenye nafaka ya mahindi yamekatwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Tarime na Rorya kwa madai ya kuingiza nafaka hiyo kutoka nje ya nchi bila kufuata taratibu.

Umoja wa Wafanyabiashara,Wakulima na Wadau wa Chakula wa wilaya ya Tarime wamelalamikia hatua hiyo kwa madai kuwa mahindi hayo yamekuwa yakinunuliwa katika vijiji ndani ya wilaya ya Tarime ili yauuzwe katika maeneo yenye njaa ndani na nje ya mkoa wa Mara lakini Polisi na TRA wameyakata kwa madai kuwa yametoka nje ya nchi

Katika barua yao kwenda Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime,TRA, mamlaka ya chakula na dawa TFDA na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya Tarime,umoja huo umetaka kupewa ufafanuzi juu ya kukamatwa kwa nafaka hiyo wakati ikiwa ndani ya nchi.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na katibu wa Umoja huo Chacha Suguta,ambayo BLOG HII imepata nakala yake imetaka kupata ufafanuzi kama kuna zuio lolote lililotolewa rasmi na Wizara ya Kilimo na Chakula kwaajili ya kuendesha zoezi hilo la kuzuia kuuzwa maeneo mengine ya nchi yenye njaa chakula hicho.

Aidha wamesema kuwa hatua hiyo pia inalenga kuwanyima haki wafanyabiahara,wakulima na wadau wa nafaka jambo ambalo pia litawafanya wapate hasara kubwa.

Kwa mujibu wa barua hiyo umoja huo umedai kuwa umeambiwa kuwa mahindi hayo yana sumu na kwamba hayapaswi kuuzwa katika maeneo mengine jambo ambalo wamepinga na kuitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa kauli hiyo.

“Sisi tuna nunua mahindi kutoka katika meneo ya Vijijini kwenye maghala na tunafuata taratibu zote za usafirishaji ikiwemo kulipia ushuru wa mazao katika maeneo husika sasa tunashangaa (TRA) kuhusika na kusafirishwa mahindi,

"Mara ya kwanza tuliambiwa yanatoka Kenye tulipowabana huku tukionyesha vibali na barua toka katika vijiji tena leo wanazuka na jambo la sumu je TFDA inafanya kazi gani na ni kwanini wasichunguze kuthibitisha kauli yao”ilisema barua hiyo na kuongeza.

“Kule mpakani kuna ulinzi mkali na kila mamlaka ipo iweje mahindi yakamatiwe kilometa 70 toka mpakani na kurejeshwa wakidai tumepitisha njia za panya….wakati ule walizuia tusiuze chakula Kenye leo tunanunua vijijini na kupeleka ndani ya nchi mikoa ya Mwanza na Shinyanga tena tunakamatwa je Tarime ni kisiwa”walihoji.

“Tunaomba ufafanuzi wa kimaandishi kwa maana ni jambo geni kwetu la TRA kushikilia magari yetu na wakitutaka tulipe Dolla 5000 kwa kila gari sawa na Shilingi Milioni nane na watupe walaka unaopelekea kutozwa faini hiyo,”ilisema sehemu ya barua hiyo.

Suguta kupitia barua hiyo  wamedai kuwa wameshikiliwa katika mpaka wa Sirari kwa zaidi ya siku sita sasa huku wengi wao wakiwa wameishiwa hata pesa ya kula na kuwafanya kuishi maisha ya tabu katika maeneo hayo na kuomba mamlaka za juu kulipatia ufumbuzi suala hilo.

‘’Ikumbukwe nyaraka zote zinazostahili na zinazoturuhusu sisi kufanya kazi hii halali ili kujipatia kipato tunazo lakini pia stakabadhi za ushuru wa Halimashauri tunazo ikiwa ni pamoja na uthibitisho wa vibali mbalimbali vya watendaji wa Serikali ya Vijiji sasa iweje tunanyanyaswa na Maafisa wa TRA,”ilisema sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo akizungumzia suala hilo Meneja wa TRA Mkoa wa Mara Joseph Kalinga alisema magari hayo yamekamatwa kutokana na kuingiza nafaka hiyo bila kufuata sheria.

“Sheria inataka kila kitu kipite katika lango la mpaka hata kama hakitozwi kodi wala ushuru lakini wenzetu wanatumia njia za panya kuingiza nafaka toka nje ya nchi”alisema Kalinga na kuongeza.

“Huwezi kuingiza chakula kwa njia za panya bila kuangaliwa ubora wake hawa jamaa wanadanganya tu na barua hizo za watendaji,tumefanya uchunguzi mahindi hayo yametoka Kenya kwa njia za panya sasa kufanya hivyo ni kuvunja Sheria na tutawatoza faini kulingana na sheria ya forodha ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2004”alisema.

“Ni kweli magari hayo yamekamatwa na bado oparesheni inaendelea kwa wale wote wanaoingiza mizigo kwa njia ya magendo hata kama hakilipiwi kodi lazima sheria zifuatwe na si vinginevyo”alisisitiza Kalinga.

“Hivyo vibari vya Vijiji walivyo navyo ni danganya toto laiti kama wangekuwa wamefata taratibu zinazotakiwa hakuna sababu ambazo zingefanya wakamatwe wamekamatwa kwa kuwa hawajafata taratibu,”aliongeza.

Hata hivyo alisema licha ya upana wa mpaka wa Tanzania na Kenya Sirari maafisa wa forodha katika mpaka huo wamekuwa wakijitoa muanga kwaajili ya kuhakikisha taifa linakusanya mapato yake ingawa wamekuwa wakipata vitisho na kufanya kazi katika mazingira magumu.

Kalinga aliwaomba wafanyabiashara ambao wanadhani endapo wanapata usumbufu wakati wakipitisha bidhaa ambazo hazilipiwi kodi wala ushuru katika lango la mpaka huo kutoa taarifa kwake ama kwa mamlaka nyingine zilizopo ili kuhakikisha kila mtu anafuata sheria za nchi,zikiwemo zile za afrika mashariki.

Sheria ya forodha ya afrika mashariki ya mwaka 2004 pamoja na mambo mengine inatoa fursa kwa mamlaka kutoza faini kulingana thamani ya mzigo na msafirishaji pia kutozwa faini hadi kufikia dolla 5000 kwa mtu yoyote anabainika kupitisha bidhaa kwa njia za panya.

Mwisho

Post a Comment