0
MENEJA MASOKO WA TBL MKOA WA MARA POLYCALIPO MAKUNJA BAADA YA KUSHAMBULIWA NA ASKARI POLISI MJINI MUSOMA

POLY AKIWA KATIKA MAJUKUMU YA KAZI

   Na Shomari Binda
        Musoma,

Askari Polisi Kituo cha Musoma jana walimshambulia kwa kumpa kichapo Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Mkoa wa Mara Polycalipo Makunja nje ya Kituo Kikuu Mjini hapa  kwa kile kilichodaiwa kutaka kumsaidia Meneja wa Mamlaka ya Usafirishaji  Majini na Nchi kavu (Sumatra) baada ya kudaiwa kuzui gari la Polisi kupita barabarani.

Akizungumzia kisa hicho ambacho kilipelekea kuvunjiwa miwani ya kusomea,kupoteza simu ya Nokia,Cheni na kuchaniwa shati vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni moja,Polycalipo alisema alishangazwa na hatua ya Jeshi la Polisi kutumia nguvu hata mahala pasipo stahili kwa kuwa hakukuwa na fujo zozote ambazo zilipelekea yeye kushambuliwa na kupigwa na askari waliokuwa zamu katika kituo hicho.

Alisema alifika katika kituo hicho majira ya saa 4 usiku akimfatilia Meneja wa Sumatra Mkoa wa Mara ambaye alikamatwa muda mchache na askari waliokuwa doria katika barabara ya Nyerere nje ya Bar ya Keryo ambaye alikuwa akiondoka kuelekea nyumbani baada ya kumaliza mazungumzo yao baada ya kukutana katika maeneo hayo.

"Mimi nilifika katika kituo cha Polisi Musoma kutaka kufahamishwa sababu ambazo zilipelekea mwenzangu ambaye nilikuwa nimekaa naye kukamatwa muda mchache baada ya kuniaga kuwa anakwenda nyumbani lakini nilishitukia nikishambuliwa na wale askari kwa hoja kuwa nimefata nini pale.

"Kwa kweli imenisikitisha nguvu ambazo zinatumiwa na askari katika kutimiza wajibu wao hata pale mtu anapoamua kutii amri ama kutaka kupata msaada kutoka katika chombo hiki cha umma ambacho ni sehemu ya huduma wahusika wanakitumia visivyo,"alisema Meneja huyo.

Alisema hoja ya Askari waliomkamata Meneja wa Sumatra kuwa aliwazui askari kupita si ya kweli bali kutokana na malori makubwa matatu yaliyokamatwa kwa kusafirisha mahindi kinyume cha utaratibu yaliyokuwa maeneo hayo yalisababisha msongamano katika barabara hiyo.

Alidai kuna kila sababu Jeshi la Polisi katika mabolesho yake kutoa elimu kwa Askari kuyajua majukumu yao ila Jamii iendelee kuliheshimu Jeshi hilo kuliko utaratibu ambao wanautumia kwa sasa kutumia nguvu kwa kila jambo hata pale mtu anapotaka msaada kutoka kwao wakiwa kama walinzi wa Raia ma Mali zao.

"Nimeamini wapo watu wanaonewa na Askari wa Jeshi la Polisi wasiojua majukumu yao pale Raia wanapowafata kupata msaada kwao kutokana na tukio hili ambalo limenikuta kwa kupigwa na kualibiwa vitu vyangu nje ya kituo cha Polisi nikiwa nahitaji ufafanuzi,"aliongeza Meneja huyo wa Masoko wa TBL.

Kutokana na kutaka kufungua mashitaka kwa thamani alizopoteza akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi,Polycalipo alisema ameamua kuachana na kufungua kesi baada ya kupata ushauri kutoka kwa viongozi huku akisisitiza mabolesho yanayofanywa na Jeshi hilo liangalie pia katika kuwapa elimu Askari wake. 
     

Post a Comment