1

    Na Shomari Binda
          Musoma,

Uongozi wa timu ya maafande wa Polisi Mara inayoshiriki ligi daraja la kwanza imewataka wachezaji wote wa timu hiyo ambao bado hawajajiunga katika mazoezi ya maandalizi ya mzunguko wa pili kufanya hivyo ili kuweza kufanya mazoezi ya pamoja.

Akizungumza na Waandishi wa Habari,Katibu Mkuu wa klabu hiyo Adamu Chiguma alisema baada ya mapumziko kutokana na kumalizika kwa mzunguko wa kwanza bado kuna wachezaji ambao hawajawasili katika mazoezi ya timu hiyo tangu yalipoanza majuma matatu yaliyopita.

Alisema ni muhimu kwa wachezaji wote kufanya mazoezi ya pamoja ili kuweza kukabiliana na mzunguko wa pili wakiwa kitu kimoja kutokana na kila timu kupania mzunguko huo ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza ligi kuu msimu ujao pamoja na kuepuka kushuka daraja.

Chiguma alisema licha ya kuweepo na changamoto mbalimbali katika klabu hiyo ikiwemo baadhi ya wachezaji kudai fedha zao za usajili lakini ni vyema kufika katika mazoezi na kuweza kuzungumza kwa pamoja ili kuweza kuunda kitu kimoja katika timu.

Alisema amepata taarifa zisizo rasmi kuwa kuna baadhi ya wachezaji ambao wameshindwa kujiunga na timu hiyo kwa madai ya kutaka fedha zao za usajili ambazo walihaidiwa kupata mara baada ya kumalizikakwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Katibu wa maafande hao wa Polisi Mara ambao wanashika nafasi ya tano katika msimamo wa kundi c linaloongozwa na timu ya Rhino ya Tabora alisema kila kitu kinaweza kuzungumzika na kufikia muafaka hivyo wachezaji ambao bado hawajajiunga kwa madai ya kutaka feha za usajili huku wakiwa hawaonekani wanakuwa hawatendi haki.

Katika hatua nyingine Chiguma amewaomba wadau wa soka katika Mkoa wa Mara kuichulia timu hiyo kuwa ni timu ya Mkoa mzima wa Mara hivyo kuwa nayo karibu na kuweza kusaidia katika matatizo mbalimbali ambayo yanaikabili timu hiyo kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi daraja la kwanza ambayo tayari imekwisha tangazwa na TFF kuanza kutimua vumbi Februari 2.

Alisema kwa kuanzia timu hiyo inahitaji zaidi ya shilingi milioni 15 ili kujipanga na kuanza mzunguko wa lala salama wa ligi hiyo ambayo imekuwa na ushindani huku kila timu kwa sasa ikionekana kuwa katika maandalizi mazito ili kuweza kukabiliana na mikikimikiki ya ligi hiyo. 

Post a Comment