0

Na Shomari Binda
     Serengeti,

WANANCHI wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamedai kuwa kutosomwa kwa taarifa za mapato na matumizi ya michango yao katika mfuko wa afya ya jamii CHF ni moja ya sababu kubwa ambayo imewakatisha tamaa kuendelea kuchangia mfuko huo.

Walisema pamoja na mfuko huo kuonyesha manufaa makubwa  baada ya kuanzishwa kwake mwaka 2004 kwa kuboresha huduma za  afya hasa katika upatikanaji wa dawa maeneo ya vijijini lakini kitendo cha Serikali za vijiji na kamati za afya za vijiji kushindwa kutoa taarifa hizo kumewakatisha tamaa wananchi wengi kujiunga na mfuko huo huku wale walikuwa wanachama wakishindwa kuendelea kiachangiaji.

Katika maoni yao ambayo wameyatoa kwa nyakati wakiti wakizungumza na waandishi wa habari ambao wako katika wilaya hiyo na wilaya Rorya kufanya utafiti wa huduma za afya zinazotolewa kupitia CHF na mfuko wa taifa wa bima ya afya,wananchi walisema pomoja na kuhitajika elimu zaidi lakini tatizo la kukosekana kwa uwazi kwa fedha za mfuko huo ni moja ya changamoto kubwa zinazoukabili mfuko huo.

“Huu mfuko wa afya ya jamii wakati unaanzishwa kwa kweli tuliona ni mkombozi mkubwa kwetu kwani tulipoambiwa tunachangia elfu tano mwaka mzima na tunapata matibabu watu sita hadi nane wakiwemo baba na mama wananchi wengi tulijiunga lakini sasa wengi tumekata tamaa kwa vile hatupati dawa pia hatusomewi taarifa za michango yetu”alisema Mzee Jackson Mteba mkazi wa kijiji cha Bwitengi.

Naye Joyce Manchati mkazi wa kijiji cha Robanda,alisema kuwa sababu nyingine kubwa ambayo pia imesababisha wananchi wengi kushindwa kuendelea kuchagia mfuko ni ukosefu wa dawa katika Zahanati na vituo vya afya katika maeneo ya vijijini.

“Unakuta umechangia elfu tano ili familia iweze kupata matibabu mwaka mzima lakini ukifika tu katika kituo unaambiwa hakuna dawa tunalazimika kwenda hospitali ya wilaya kule Nyerere DDH au kwenda kununua dawa katika maduka binafsi sasa yanini nitoe elfu tano zangu bila kuona faida”alisema Joyce.

Kauli hiyo ya Joyece imeongwa mkono na mkazi mwingine wa kijiji cha NataMbiso William Mahela ambaye amedai kuwa tangu familia yake ichangie kiasi hicho cha fedha katika mfuko huo kwa miaka mitatu mfululizo hakuna hata siku moja iliwahi kupata huduma katika kituo cha afya katika eneo hilo kwa kukosa dawa hatua ambayo imemfanya kujiondoa kuwa mwanachama wa mfuko huo.

“Kila tukienda pale kituoni hata kama ni ugonjwa wa Malaria unaambiwa hakuna dawa na kutakiwa ukanunue katika maduka ya dawa sasa iweje niendelee kuwa mchangiaji bila ya kuona manufaa lakini pia hakuna hata siku tuliwahi kupewa taarifa za mapato na matumizi ya michango yetu”alisema Mahela.

Hata hivyo idadi kubwa ya wananchi wa wilaya ya Serengeti ambao walihojiwa kuhusu huduma za CHF walishauri Serikali kupitia halmashauri kusimamia uwazi wa michango  ya wananchi na upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya vya kutolea huduma hatua ambayo walisema itawezesha wananchi wengi kuvutiwa kujiunga na mifuko hiyo.

Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya Serengeti Dk Salum Manyata,alisema mfuko wa CHF umekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo elimu ndogo kwa wananchi na kutokuwepo kwa utashi wa kisiasa katika kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo.

Taarifa ya mganga huyo wa wilaya ya Serengeti ambayo ilisomwa na kaimu mratibu wa mfuko Dk Shadraka Isaro mbele ya waandishi wa habari wanaofanya utafiti huo,alisema changamoto hizo zimesababisha wanachama wa mfuko huo kupungua kutoka 5,210 waliokuwepo mwaka 2004 wakati mfuko huo ukianzishwa hadi kufikia 485 mwezi Mei mwaka 2012.

“Wakati wa utekelezaji wa mfuko huu wa afya ya jamii,changamoto nyingi zimejitokeza hivyo kufanya idadi ya wanachama wake kushuka toka 5,210 mwaka 2004 hadi kufikia 485 mwezi mei mwaka 2012 lakini pia tatizo la uelewa mdogo wa jamii juu ya mfuko huu na dhana ya ushirikishwaji,umiliki na usimamizi wa huduma za afya ni miongini mwa changamoto tulizozibaini”alisema mganga huyo mkuu wa Serengeti.

Hata hivyo kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Serengeti  Salvanus Lugira,amekiri mfuko wa CHF kukabiliwa na changamoto nyingi huku akisema tayari halmashauri imetoa waraka wa kuzitaka serikali za vijiji kutoa mapato na matumizi katika vijiji vyao ikiwemo michango hiyo ya wananchi kuhusu mfuko huo huku viongozi wa kisiasa wakitakiwa kufanya uhamasishaji mkubwa kwa wananchi katika kujiunga na CHF.

Post a Comment