0
Na Shomari Binda
        Bunda,

WAKULIMA wa wilaya ya Bunda Mkoani Mara,wameanza kuachana na kilimo cha zao la pamba na hivyo kuelekeza nguvu zao katika kilimo cha mazao ya Mpunga na Mahindi ikiwa ni mwaka mmoja tu baada  ya kushuka kwa bei ya zao la Pamba katika soko la dunia hatua ambayo idaiwa kuwasababishia hasara kubwa.

Baadhi ya wakulima hao ambao sasa wanatumia mabonde  yaliomo ndani ya wilaya hiyo kulima mazao hayo kama mazao mbadala  ya biashara na chakula wamemueleza mkuu wa wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe kuwa hatua hiyo ya kuachana na kilimo cha pamba imetokana na hasara kubwa ambayo wameipata katika msimu wa mwaka jana wa zao hilo.

Walisema mbali na kutumia fedha nyingi katika kilimo cha zao la pamba lakini pia Serikali imeshindwa kuwapa mikopo ya zana za kisasa za kilimo kwaajili ya kilimo cha pamba jambo ambalo limewafanya kuachana na kilimo hicho hivyo kuelekeza nguvu zao katika kilimo cha mpunga na mahindi kwa kutumia jembe la mkono.

''Inakuwa haina maana ya kuendelea na kilimo cha zao hili kwani hakina manufaa kwetu tunatumia fedha nyingi katika kilimo hadi nyakani za mavuno lakini thamani ya mauzo inakuwa haikidhi.

"Ni bora tuelekeze nguvu zetu katika kilimo cha mazo mengine na pale Serikali itakapoona faida ya kilimo cha pamba kwa ajili ya masrahi yetu na Taifa wataangalia namna ya kuwezesha hili,"walisema wakulima hao.

Hata hivyo mkaguzi wa pamba wilaya ya Bunda Bw Igoro Marongo,pamoja na kuwapongeza wananchi hao kufikiria kutafuta mazao mbadala lakini hatua hiyo isiwafanye kutoachana na kilimo cha pamba badala yake walime kwa kufuata  ushauri  wa kitaalamu  ili kuwawezesha kuzalisha  zaidi  ya kilo 1,000 kwa ekari ili kupata fedha nyingi tofauti na hivi sasa.

"Ushauri wangu ni kuwataka wakulima wasiachane na zao la pamba bali walime kitaalmu zaidi ili kupata mavuno kwa asilimia kubwa ambayo itawezesha kupata fedha nyingi,"alisema Igoro.

Kwa sababu hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe,ambaye aliwatembelea wakulima hao katika kujionea kilimo hicho,amewaagiza maafisa kilimo katika ngazi ya Kata na Wilaya kuhamasisha  wakulima kuunda vikundi ambavyo vitawawezesha kupata matrekta  ya kiliomo kutoka kwa makampuni makubwa yaliopo ndani ya wilaya hiyo.

Baadhi ya mabonde ambayo yametangazwa na Mkuu wa Wilaya hiyo yatumike kwa kilimo hicho ni pamoja na Nansimo,Mwitende,Igundu,Iramba,Namuhura  pamoja na Karukekere,Bitaraguru,Mranda,Chingurubira na  Chamtigiti.

Post a Comment