0

JAMII imetakiwa kubadilika na kuachana na vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake kwani kufanya hivyo kunawafanya Wanawake kuwa wanyonge na kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato kitakachowezesha kuisadia familai.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mratibu kitengo cha Wanawake kutoka Shirika la kutetea Wanawake na Watoto la ABC Foundation Lilian Charles alipokuwa akitoa mada katika Kongamano la maazimisho ya siku ya Wanawake Duniani lililofanyika Mjini Musoma kwa kuwashirikisha Wanawake kutoka katika kata 13 za Manispaa hiyo.

Alisema katika siku za hivi karibuni kupitia Shirika hilo matukio mbalimbali ya Ukatili na Unyanyasaji wa Wanawake yameripotiwa mara kwa mara hali ambayo imekuwa ikikwamisha jitihada za kumkomboa Mwanamke kutokana na vitendo hivyo ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikimnyongonyesha.

Lilian alidai Jamii nzima inapaswa kutambua umuhimu wa Mwanamke katika familia kwa kuwa mlezi mkuu hivyo kufanyiwa unyanyasaji kunakwamisha Maendeleo na hivyo kuendelea kuwa na maisha duni na mambo mengi kukwama kwa kushindwa kujishughulisha vyema katika majukumu.

"Matukio ya Unyanyasaji wa Wanawake katika Jamii bado yanaendeea kufanyika,na hii inaendelea kukwamisha jitihada za wadau mbalimbali katika kuondosha hali hii na hili sio jukumu la watu wachache bali kila mmoja anapaswa kukemea Unyanyasaji pale anapoona hali hii inatokea"alisema Lilian.

Awali akifungua Kongomano hilo,mdau katika Maendeleo ya Mama na Jamii Regina Andrea alitumia siku ya Wanawake Duniani kulaani vitendo vya Mauaji ya Wanawake kwa kukatwa vichwa kwa imani ya kishirikina yaliyokuwa yakitokea mkoani Mara hivi karibuni na kuwatia hofu Wanawake.

Alisema vitendo hivyo viliwafanya Wanawake kushindwa kufanya majukumu yao ipasavyo ya kujiongezea kipato katika familia zao kutokana na hofu ya kufanyiwa vitendo vya Ukatili na kutoa wito kwa Jamii kukataa vitendo hivyo na kuisaidia Serikali kuwafichua wahusika pale vitendo kama hivyo vitakapojitokeza tena.

Kuhusu malezi ya Watoto,Regina alisema licha ya Wanawake kuwa na majukumu mengi wasisahau jukumu la kuwalea watoto katika maadili mazuri kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili ambao kwa kiasi kikubwa umeongezeka katika Taifa na kusema kuwa hali hiyo ikiachwa iendelee kutazalishwa Taifa la watu wasio kuwa na maadili.

Alisema ni muhimu kuwahimiza Watoto hasa wa kike kuzingatia suala la elimu kwa kuwa litakuja kuwakomboa hapo baadae kwani dunia ya sasa pasi kuwa na elimu bora huwezi kwenda na kasi ya Maendeleo hasa baada ya kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao soko la ajira limekuwa na ushindani mkubwa ambapo huwezi kuingia bila kuwa na elimu bora.

Aidha mdau huyo wa Maendeleo ya Wanawake,aliwataka Wanawake kuchangamkia fursa za Maendeleo kwa kujitoa kujishughulisha ili kuweza kuongeza kipato ambacho kwa namna moja kitampa heshima Mwanamke na kuacha kuwa tegemezi kwa kila jambo ambalo anataka kulifanya katika familia.

Kauli mbiu ya siku ya Wanawake Duniani mwaka huu inasema kuwa,Uelewa wa masuala ya kijinsia ongeza kasi"ambayo inasisitiza umuhimu wa kuhamasisha na kuelimisha Jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia maswala ya kijinsia katika kuleta Maendeleo ya Wanawake na Jamii.

Post a Comment