Tume
ya Taifa iliyoundwa na Mh. Waziri mkuu Mizengo Pinda kuchunguza kushuka
kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012
imewaomba watanzania kuipa ushirikiano kwa kutoa maoni yao ili iweze
kukamilisha majukumu iliyopewa kwa muda na ufanisi mkubwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo
Prof.Sifuni Mchome ameeleza kuwa tume hiyo ilianza kazi mara baada ya
kuzinduliwa na Waziri mkuu tarehe 2 mwezi Machi mwaka huu na kufafanua
kuwa jukumu lililopo sasa ni kuanza kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa
watanzania ili kubaini sababu za matokeo mabaya ya mtihani huo.
Amesema kuwa
tume hiyo pamoja na mambo mengine imepewa jukumu la kutoa mapendekezo
ya hatua za kuchukua ili kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka
kwa kiwango cha elimu nchini huku mapendekezo hayo yakizingatia kipindi
cha muda mfupi , kati na kipindi cha muda mrefu.
Prof.
Sifuni ameeleza kuwa tume hiyo inafanya kazi kwa kuzingatia
hadidu mbalimbali za rejea zikiwemo kubainisha sababu za matokeo mabaya
ya kidato cha nne 2012, sababu za kushuka kwa kiwango cha
ufaulu, nafasi ya Halmashauri katika kusimamia elimu ya sekondari katika
halmashauri zake.
Rejea
nyingine ni pamoja na pamoja na kuanisha sababu nyingine zinazoweza
kuwa zimechangia hali ya matokeo hayo pamoja na kutoa mapendekezo ya
hatua za kuchukua mara moja kwa wanafunzi 240,903 waliofeli mitihani yao
kwa kupata daraja sifuri.
Amefafanua
kuwa tume katika kutekeleza majukumu yake itapitia mitaala na
mihutasari ya Elimu ya Msingi na Sekondari, kutathimini kiwango na
mazingira ya ufundishaji na ufunzaji, kuangalia mfumo wa upimaji na
tathmini ya mitihani pia usimamizi na uendeshaji.
Pia pamoja na mambo mengine tume itatathmini mchango wa jamii na wazazi/ walezi katika maendeleo ya wanafunzi, hali ya upatikanaji wa chakula cha mchana, upungufu wa majengo ya shule,madarasa, maabara na maktaba.
Imeandikwa na Alon Msigwa wa Idara ya Habari Maelezo
Post a Comment
0 comments