0
MKOA wa Mara umeandaa mkakati wa miaka mitatu wenye lengo la kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi pamoja na kubolesha afya za walioathirika na ugonjwa huo ili kuweza kuokoa nguvu kazi ya Taifa inayoangamia kutokana na ugonjwa huo.

Akizungumza na Blog hii Ofisini kwake,Mganga mkuu wa Hospitali ya mkoa wa Mara Dk.Samsoni Wenani alisema mkakati huo ni endelevu ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa la kupambana na ugonjwa huo linafanikiwa kubwa ikiwa kupunguza maambukizi mapya ambayo imeonekana bado yapo katika maeneo mbalimbali.

Alisema moja ya mkakati huo ni kutoa elimu ya VVU na Ukimwi katika Vijiji,Tarafa na Mitaa ili kuhakikisha kila mmoja anafahamu athari za ugonjwa huo na kujiepusha kupata ugonjwa huo na hivyo kupunguza nguvu kazi katika uwajibikaji wa kujiletea Maendeleo katika Jamii  na Taifa.

Winani alisema katika mkakati huo ni kuongeza vituo vya upimaji (PMTCT) kutoka 198 hadi 275 pamoja na kuongeza vituo vya kutolea dawa ya kupunguza makali ya VVU kutoka 45 hadi 94 katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mara na kuimalisha uratibu na usimamizi wa shughuli za Ukimwi katika ngazi ya Wilaya na Mkoa.

"Kikao cha wadau walio katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi mkoa wa Mara kimefanyika na kila mdau amepangiwa majukumu ya kutekeleza na baada ya miezi sita kikao hicho kitafanyika tena kutathimini mafanikio na changamoto na kujipanga vizuri ili kufikia malengo.

"Kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2008,watu walioambukizwa VVU mkoa wa Mara ni asilimia 7.7 na kuwa katika nafasi ya nne kitaifa kwa kuwa na asilimia kubwa ya maambukizi ya VVU hivyo lazima tuwe na jitihada za makusudi kukabiliana na hali iliyopo.

" Kutokana na hali hii mkoa unafanya juhudi maalum za kupunguza maambukizi mapya ya VVU na vifo vinavyotokana na Ukimwi katika mkoa wa Mara na huu ni mkakati ambao kila mmoja anapaswa kushiriki na sio kuwaachia madaktari ama wadau wa mapambano dhidi ya Ukimwi,"alisema Wenani.

Alisema katika mkakati huo wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kujitokeza kupima kwa hiari na kuweza kupata ushauri unaofaa mara baada ya vipimo na kuweza kuishi kwa matumaini hata kama vipimo vitaonyesha kuathirika.

Mganga Mkuu wa mkoa wa Mara aliongeza kuwa ndani ya mkakati huo kipaumbele kimewekwa kutoa elimu zaidi katika maeneo ya mialo na migodin kutokana na maeneo hayo kuwa na muingilino mkubwa wa watu katika shughuli za kujitafutia kipato na hivyo kuwa katika hali hatarishi ya maambukizi ya Ukimwi.  

Post a Comment