Naibu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Ummy Mwalimu amewataka
wanawake nchini kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo
zinazojitokeza katika maeneo yao ili waweze kujikwamua kiuchumi na
kupambana na umaskini.
Kauli
hiyo ameitoa leo jijini Dar es salaam wakati akitoa ufafanuzi wa
masuala mbalimbali kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani yatakayofanyika machi 7 mwaka huu.
Amesema
maadhimisho hayo yanalenga kuwezesha upimaji wa utekelezaji wa maazimio ,
matamko, mikataba na itifiki mbalimbali za kimataifa na kikanda
zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia kwa wanawake na kubainisha
kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kauli mbiu isemayo Uelewa wa Masuala ya Jinsia katika Jamii; Ongeza kasi“
Amesema
serikali ya Tanzania imekuwa na mipango thabiti ya kuhakikisha kuwa
usawa wa kijinsia nchini unazingatiwa kwa kuchukua hatua mbalimbali
zikiwemo kuridhia na kusaini mikataba, itifaki, maazimio na matamko
mbalimbali yanayohusu maendeleo, haki na ustawi wa wanawake na utungaji
wa sheria ya Ardhi Na. 4 na ile ya vijiji Na.5 za mwaka 1999 ambazo
zinatoa fursa sawa za umiliki wa ardhi.
Bi
Ummy amefafanua kuwa kuwa Tanzania imeshasaini na kuridhia mkataba wa
kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW 1979), Azimio la
ulingo wa Beijing (1995), mkataba wa malengo ya Milenia,
Azimio la
kuleta Usawa wa Kijinsia katika nchi za Afrika (2004) na Mkataba wa
Afrika wa Haki za Binadamu za Wanawake (2006).
Mikataba
mingine iliyosainiwa na kuridhiwa na Tanzania ni ule wa Itifaki ya
Maendeleo ya Jinsia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC 2008).
Ameeleza
kuwa serikali imepitisha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya
Mwaka 2000 ili kutoa mwongozo wa kuratibu uingizwaji wa masuala ya
jinsia katika mipango, Sera, Programu, mikakati na bajeti za kisekta ili
kuleta usawa baina ya wanawake na wanaume katika masuala ya maendeleo
nchini.
Pia amefafanua kuwa Wizara yake imeratibu kuanzishwa
kwa dawati la jinsia katika Wizara, Idara za serikali zinazojitegemea,
sekretarieti za mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini ili kuharakisha
utekelezaji wa masuala ya jinsia.
Kuhusu
mafanikio ya kuleta usawa wa kijinsia nchini Bi. Ummy ameeleza kuwa
kumekuwa na ongezeko la wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi
zikiwemo uwakilishi wa wanawake bungeni kutoka asilimia 30 mwaka 2005 na
kufikia 36 mwaka 2010.
“Napenda
kueleza kuwa mafanikio haya kwa wanawake katika ngazi za maamuzi nchini
ni makubwa kwa sasa ukilinganisha na miaka iliyopita, sasa tuna mawaziri
wanawake, tuna wakuu wa mikoa na wilaya , tuna wabunge wengi tu ,
Majaji wa mahakama kuu, makatibu wakuu na viongozi wengi wanawake”
amesema.
Aidha
amefafanua kuwa serikali imeendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi na
tayari imeratibu na kusimamia mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) na
kuongeza kuwa wanawake wamewezeshwa kiuchumi kwa kuwapatia elimu, mbinu
za ujasiriamali na mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya Wanawake
Tanzania ambapo mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa
wanawake 5270 na wanaume 1157.
Ameeleza
kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana bado wanawake nchini
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa uwepo wa wasichana
wanaokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba za
utotoni na kuwepo kwa vtendo vya ukatili wa kijinsia katika baadhi ya
jamii nchini.
Imeandikwa na Alon Msigwa wa Idara ya Habari Maelezo
Post a Comment
0 comments