0


MWANAMKE kikongwe mwenye umri wa miaka 72 ameuawa na watu  wasiofahamika kisha kumzika katika shimo lenye urefu wa futi moja huku kichwa na miguu vikibaki bila kufukiwa katika mtaa wa Bukanga Kata ya Makoko Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa SACP Absalom  Mwakyoma alisema kuwa tukio hilo lilijulikana baada ya kuonekana marehemu huyo machi 26 mwaka huu majira ya 12:30 asubuhi akiwa shambani kwake.

Kamanda alimtaja marehemu kuwa ni Nyamakafu Patrick (72) ambae alikuwa ni mkazi wa kijiji cha Bukanga kata ya Makoko tarafa ya Musoma mjini ambae alikuwa anajiuhusisha na shughuli za kilimo.

Aidha alisema kuwa marehemu kabla ya kuuawa aliondoka nyumbani kwake kuelekea shambani ambapo hulima kisha kurejea nyumbani jioni lakini marehemu huyo hakuweza kurudi siku hiyo jambo ambalo lilimtia mashaka mume wa marehemu huyo  Msira Masige pamoja na watoto wake.

Alisema baada ya familiya hiyo kuingiwa hofu walichukua jukumu la kumtafuta ambapo siku iliyofuata waliwahi katika shamba lao na kumpata marehemu akiwa kauawa kwa kufungwa kanga shingoni kisha kufukiwa na baadhi ya sehemu zikiwa nje.

Kamanda alisema kuwa hakuna mtu au watu wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kuhusina na tukio hilo na kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.

Hata hivyo kamanda alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hosptali ya mkoa wa Mara kwa lengo la kuendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na mauaji hayo.

Mwakayoma alitoa wito kwa Wananchi watakaopata taarifa kuhusiana na tukio hilo kutoa taarifa katika Jeshi la Polisi ili wale watakaobainika kuhusika na tukio hilo waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.


 

Post a Comment