0


KIPA wa zamani wa timu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stras Mfaume Athumani amealikwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara kuhamasisha mchezo wa soka na kuunda timu ya mkoa ambayo itakuwa na nguvu na kuutangaza mkoa kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Katika mkutano wake na Wandishi wa Habari,Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Christopher Sanya pamoja na mambo mengine amezungumzia suala la michezo na kudai ili kuona Mara inajitangaza vyema kupitia michezo ameona kuna umuhimu wa kuanzisha jitihada mbalimbali ili kufikia adhima hiyo.

Alisema katika kipindi cha miaka ya nyuma mkoa wa Mara umekuwa ukisifikia kwa kuibua viapaji mbalimbali kupitia michezo ya riadha,mpira wa mikono,bao,mpira wa miguu pamoja na michezo mingine lakini kwa sasa imeonekana nguvu na hamasa imepungua hivyo kuamua kuangalia upande huo kwa namana nyingine ya kuinua.

Sanya alidai moja ya mambo ambayo amekusudia kuyapa kipaumbele ni suala la kuweka watu pamoja kupitia michezo na kwa kuanzia anaanzia na upande wa soka na akiwa kama Mwenyekiti wa CCM mkoa atashirikiana na viongozi wengine kuinua kiwango cha soka mkoani pamoja na michezo mingine.

"Nimeshazungumza na Mfaume kipa wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa Stars...mchango wake katika soka la Tanzania unafahamika na tumeshazungumza na kukubaliana hivyo atafika hapa mkoani wiki ijayo tutakutana na viongopzi wa soka mkoa kuona namna ambayo mpango huu utafanikiwa.

"Lengo pia ni kuhakikisha soka la vijana linahamasishwa kila Wilaya maana nchi zote zilizoendelea ki soka zimewekeza katika soka la vijana tangu zamani na sisi hatujachelewa sana maana kumekuwa na mashindano ya kila mwaka ya copa coca cola na tumekuwa tukishiriki naamini Mfaume atakuja kuongeza hamasa zaidi,"alisema Sanya.

Aidha Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Mara alisema pamoja na kuangalia soka la vijana pia mchezaji huyo wa zamani wa Taifa Stars atakuwa na jukumu la kushirikiana na wadau wengine wa soka mkoani Mara kuhakikisha kinaundwa kikosi bora cha mkoa ambacho kitakuwa kikishiriki mashindano mbalimbali ya kitaifa na michezo mingine kuvisaidia vilabu mbinu za kufanya vizuri katika ligi wanazoshiriki.

Wakati huo huo Sanya ameipongeza timu ya Polisi Bunda kwa kuchukua ubingwa wa mkoa wa Mara katika ligi iliyomalizika hivi karibuni na kuwaomba wadau wa soka kuiunga mkono timu hiyo katika maandalizi yake kwa ajili kwenda kushiriki ligi ya kanda ili iweze kufanya vizuri na kuendelea kuutangaza mkoa wa Mara kupitia michezo.

Post a Comment