0
MTU mmoja mkazi wa kata ya Nyamatare Manispaa ya Musoma John Katute (56),amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara akituhumiwa kwa kosa la kuharibu miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Musoma (MUWASA) na kusababisha usumbufu kwa watumiaji.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Faisal Kahamba,imedaiwa na mwendesha mashitaka wa Mahakama hiyo Jonas Kaijage mtuhumiwa alifanya kosa hilo katika maeneo hayo ya Nyamatare tarehe 13 machi 2013.

Mahakama ilielezwa na mwendesha mashitaka huyo,mtuhumiwa amefanya kosa hilo kinyume na kifungu namba 47 kifungu kidogo cha (1) na (2) ya sheria ya usambazaji wa maji namba 12 ya mwaka 2009.

Kaijage ameiambia Mahakama upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika ili mtuhumiwa wa kosa hilo la kuharibu miundombinu ya usambazaji wa maji katika Manispaa ya Musoma ianze kusikilizwa.

Mtuhumiwa wa kosa hilo yuko nje kwa dhamana ya watu wawili kwa kiasi cha shilingi milioni mbili kila mmoja huku kesi hiyo ikipangwa kusikilizwa tena aprili 30.

Post a Comment