TARIME KUTENGENEZWA UWANJA WA MPIRA
HALIMASHAURI ya Wilaya ya Tarime imepanga kutenga fedha kwa ajili ya marekebisho ya uwanja wa michezo wa Sabasaba uliopo mjini humo ili kuwafanya vijana kuwa na hamu ya kushiriki katika michezo katika uwanja mzuri na kuwaepusha kuwa na muda mrefu wa kukaa bila kushiriki katika michezo hali ambayo inaweza kuwafanya kwenda kushiriki katika vitendo vya kiuhalifu.
Akizungumza na Mtanzania,Mkurugenzi wa Halimashauri ya Wilaya ya Tarime Athuman Akalama alisema kutokana na maombi yaliyoombwa na Chama cha mpira wa miguu Wilayani humo (TAFA) Halimashauri imeona kuna kila sababu ya kuufanyia marekebisho makubwa uwanja huo ili michezo mbalimbali hususani soka iweze kufanyika.
Alisema katika siku za nyuma vijana wengi wamekuwa wakijitokeza katika uwanja huo na na kushiriki michezo katika kipindi cha jioni lakini kwa sasa wamekuwa ni wachache wanaojitokeza kutokana na uwanja huo kutokuwa katika hali nzuri hivyo Halimashauri imeamua kuurudisha katika hali yake ya zamani.
Akalama alisema kwa kuanzia katika awamu ya kwanza watausawazisha uwanja huo kabla ya kutafuta nguvu nyingine ya fedha kwa kushirikiana na wadau wa michezo kuona namna ya kuuwekea nyasi ili kuufanya uwe na ubora zaidi na kufanyika shughuli za kimichezo.
"Uwanja wa sabasaba ulikuwa ukijaza watu wengi nyakati za jioni kwa kushiriki michezo,lakini kwa sasa muitikio umekuwa ni mdogo nadhani ni kutokana na uwanja wenyewe kutokuwa katika hali nzuri lakini Halimashauri imeeamua kutafuta fedha na kuufanyia marekebisho ili michezo ipate kuchezwa.
"Unajua inapofanyika michezo hata muda wa vijana kwenda kukaa kwenye makundi ya kiuhalifu ama uvutaji bangi unakuwa haupo hilo tumeliona na tutajitahidi kadri ya uwezo ili lengo la kuukarabati uwanja huo liweze kukamilka na kila mmoja aweze kushiriki katika michezo,"alisema Akalama.
Alisema licha ya michezo kuwaepusha vijana na makundi hatarishi pia michezo kwa sasa imekuwa ikizalisha ajira nyingi na matajiri wakubwa kwa sasa dunia ni pamoja na wanamichezo ambao wamekuwa na kipato kikubwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama mpira wa miguu Wilayani Tarime Seleriya Marayi alisema kukubali kwa Halimashauri kutengeneza uwanja huo kutarudisha nguvu na hamasa ya mchezo wa soka uliokuwepo katika Wilaya hiyo ambapo katika kipindi cha nyuma vipaji mbalimbali vya soka vilizalishwa Wilaya hapo.
Post a Comment
0 comments