BAADA
ya Serikali kubuni na kufanikiwa kuanzisha na kuendesha usafiri wa
treni jijini Dar es Salaam, sasa inajipanga kubinafsisha usafiri huo
unaosaidia kupunguza msongamano. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe, alisema hayo bungeni jana, wakati akiwasilisha makadirio ya
bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Alisema Serikali inakamilisha mchakato wa kumpata mwekezaji na mwendeshaji wa huduma hiyo jijini humo.
Kwa
mujibu wa Dk Mwakyembe, Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania
(RAHCO), ndiyo itakayokamilisha mchakato wa kumpata mwekezaji na
mwendeshaji wa huduma hiyo, atakayetumia miundombinu ya reli iliyopo na
vichwa vya treni na mabehewa maalumu ya usafiri katika miji.
Dk
Mwakyembe alisema mwitikio wa wananchi kutumia huduma ya treni ya
abiria, umekuwa mkubwa ikilinganishwa na uwezo wa kutoa huduma yenyewe,
hususan nyakati za mahitaji makubwa ya usafiri.
Wingi
wa abiria Kwa sasa kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, treni hiyo ya jijini Dar
es Salaam, inabeba watu 14,000 kwa kila siku, sawa na zaidi ya daladala
467 zenye uwezo wa kubeba abiria 30 kila siku.
“Kwa
upande wa Tazara, wastani wa idadi ya abiria wanaosafiri kwa treni kwa
siku, umefikia 9,000 baada ya kukamilika kwa ukarabati wa mabehewa
mengine saba na kichwa kimoja cha treni na kuanza kutumika rasmi Mei 9,
2013.
“Aidha,
kwa upande wa TRL, wastani wa abiria wanaosafiri kwa siku ni 5,000,”
aliongeza Dk Mwakyembe akizungumzia usafiri huo ulioanza Oktoba mwaka
jana, kati ya Stesheni na Ubungo Maziwa na kati ya Tazara na Mwakanga.
Faida,
changamoto Alisema kuanzishwa kwa usafiri huo wa treni jijini Dar es
Salaam, kumesaidia kumepunguza idadi ya magari barabarani.
“Kuanza
kwa usafiri huu, kumeshawishi baadhi ya wananchi waliokuwa wanatumia
magari binafsi kuja katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kuanza kutumia
usafiri wa treni,” alisema Dk Mwakyembe.
Alizitaja
baadhi ya faida zingine zinazotokana na usafiri huo, kuwa ni kupungua
kwa matumizi ya mafuta, muda unaotumika barabarani na hivyo kusaidia
wananchi kufika kwa wakati katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Alisema
Wizara inaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizojitokeza,
zikiwamo za kutokuwa na mfumo thabiti wa kukusanya mapato, uchakavu wa
miundombinu na uhaba wa injini na mabehewa.
Kuhusu
kuongeza huduma za usafiri huo, alisema Wizara imeunda Kamati Maalumu
chini ya uenyekiti wa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, ili
kuchambua, kuainisha na kushauri mipango na mikakati ya kuboresha na
kupanua usafiri huo.
Ruti
mpya “Pia Wizara inaangalia uwezekano wa kuanzisha huduma maalumu ya
treni kati ya Stesheni ya Dar es Salaam na Gongo la Mboto kwa ajili ya
kuhudumia abiria wanaopita kwenda Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere,” alisema Dk Mwakyembe.
Kwa
upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilishauri kuwa
ili mradi huo ufanye kazi kwa ufanisi na kuondokana na hasara, Serikali
iharakishe kununua angalau treni mbili za kisasa na maalumu kwa safari
fupi, ambazo gharama yake ni Sh bilioni 8 kila moja
CHANZO SUFIANIMAFOTOBLOG
Post a Comment
0 comments