0
MKAZI wa kata ya Nyakato katika Manispaa ya Musoma Msafiri Antony (34) aliyeachiwa na Msamaha wa Rais aprili 26 mwaka huu katika sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar amekamatwa na jeshi la polisi mkoani Mara baada ya kukutwa na marobota 2 ya nguo za kike pamoja na majola 10 ya vitambaa vya kike vinavyodaiwa kuwa vya wizi.

Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake,Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mara Afisa Mnadhimu wa polisi Paul Kasabago alisema mtuhumiwa huyo al;ikamatwa alikamatwa mei 20 akiwa katika gari namba T 974 CED Toyota Hiace ikitokea Bunda kwenda Musoma baada ya kupata taarifa kutoka kwa Wananchi wema.

Kasabago alisema mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akitumikia kifungo kutokana na kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba kabla ya kuachiwa na Rais alikuwa miongoni mwa washitakiwa wengine wawili ambao walikamatwa siku hiyo wakiwa katika gari lingine lenye namba T 547 BSF Toyota Hiace ambayo pia ilikuwa ikitoka Bunda kwenda Musoma wakiwa na bunduki aina ya S/Gun iliyotengenezwa kienyeji na risasi 3.

Kaimu kamanda huyo aliwataja watu hao ambao pia walikutwa na mafurushi 4 ya nguo mbalimbali pamoja na Tv inchi 14 kuwa ni Mwita Mkama (40)mkazi wa Tarime pamoja na Catherine Sinza (28) mkazi wa Bunda ambaye baada ya kupekuliwa maungoni mwake alikutwa na risasi 3 ndani ya chupi aliyokuwa amevaa.

"Watu hawa walikuwa kitu kimoja na walikuwa wamepanda magari hayo tofauti ili kuweza kufanikiwa kufika kule walikokuwa wakienda lakini kutokana na ushirikiano wa Wananchi kwa kutoa taarifa za siri tulifanikiwa kuweka mitego na kuwakamata na hadi sasa bado tunaendelea kuwachua maelezo na pale upelelezi utakapokamilika tutawafikisha mahakamani.

"Tunawaomba Wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuweza kukomesha watu wote ambao wanajihusisha katika vitendo vya kiuhalifu katika makazi kwa kuwa hawa wanaofanya vitendo hivi wanakaa huko na wengine wanafahamika na jeshi la polisi haliwezi kutoa siri kwa mtoa taarifa,"alisema Kasabago.

Aidha kaimu kamanda wa polisi mkoani Mara alisema katika oparesheni ambayo inaendelea katika maeneo mbalimbali walifanikiwa kumkamata mtu mmoja Adamu Maiga (30 anayetuhumiwa kutenda kosa la mauaji aprili  mosi katika Supermarket ya Cotra iliyopo Baruti katika Manispaa ya Musoma.

Katika oparesheni hiyo walikamatwa watu watatu kuhusiana na makosa ya unyang'anyi wa kutumia siraha kwenye maeneo mbalimbali Wilayani Bunda ambao bado wanaendelea kuhojiwa na jeshi la polisi na baada ya kukamilka kwa upelelezi watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili. 

Post a Comment