0

KATIKA hali isiyo ya kawaida,madiwani wa Halimashauri ya Manispaa ya Musoma juzi  waliamua kufunga geti la Halimashauri hiyo kwa kile walichodai hawawezi kwenda kwenye mapokezi ya mwenge bila kupewa posho zao kwa ajili ya mapokezi na magari ambayo wenyewe wanastahili kupanda.

Sakata hilo ambalo BLOG HII ililishuhudia lilianza majira ya saa mbili asubuhi hali iliyopelekea Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya kuamua kuondoka na kumuacha Mkurugernzi wa Manispaa ya Musoma,wakuu wa Idara pamoja na Watumishi wakiwa  wamepigwa na butwaa wasijue la kufanya.

Kamera ya Blog ilimshuhudi Naibu Meya wa Manispaa ya Musoma na Diwani wa Kata ya Mwisenge Bwire Nyamwelo (CHADEMA) akiwa amesimama katika geti la Halimashauri hiyo huku mlinzi akiwa pembeni na kuzuia magari kutokuondoka hadi pale watakapolipwa posho  za mapokezi ya mwenge.

"Hatuwezi kukubaliana na hali ya kudharauliwa,sisi kama madiwani kwanza hatuwezi kupelekwa kwenye mapokezi ya Mwenge tukiwa kwenye magari yasiyo ya Manispaa na lazima suala la posho litolewe kwanza,sio mtupeleke sisi ni viongozi tuliochaguliwa na Wananchi.

"Inakuaje mnatupatia gari la Chama cha Walimu wakati tuna magari yetu,hatuwezi kwenda huko hadi mambo haya tunayoyataka yatakaposhughulikiwa,tutatumiaje magari ya kuazima wakati tuna magari yetu hili haliwezekani na posho lazima tupewe kwanza,"alisikika Naibu Meya huyo.

Alipoulizwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma kuhusu kile kilichotokea hadi madiwani kuamua kufunga geti na kuzuia mapokezi ya Mwenge,Mkurugenzi huyo Ahmed Sawa alisema ameshangazwa na uamuzi wa madiwani na kudai kwa upande wake amefanya kila kitu kinachotakiwa katika mapokezi ya mwenge na kama wameamua kufungia magari ili mwenge usipokelewe yatakuwa ni maamuzi yao.

"Kama suala lilikuwa ni magari wanayotaka kutumia nimeamua kutoa gari la Chama cha Walimu ambalo wamelikataa na kutumiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na nimewapa gari ambalo mimi nalitumia pamoja na gari lingine la Halimashauri lakini bado wamefunga geti,kama wanahoja nyingine ya posho ni suala ambalo linashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu na kazi ndiyo inaanza mimi sina la kufanya.

"Nasikia Mwenge umeshafika eneo la mapokezi kutoka Butiama lakini bado geti limefungwa kiu kweli kwa sasa sina la kuzungumzia kuhusiana na tukio hili ila ngoja tuone hali itakavyokuwa kama wataendelea kuwa na msimamo wao.

Hata hivyo BLOG hii ilishuhudia baadhi ya madiwani wakiwa wanashauliana ili Naibu Meya aweze kuruhusu magari ambapo ilishuhudiwa baada ya muda kufungua geti na kuamua kuyaruhusu magari kuondoka yalifika katika eneo la mapokezi na kukuta tayari kukuta tayari msafara wa mbio za mwenge ukiwa umeshafika mapema kutokea Butiama.

"Kutokana na msimamo aliokuwa nao Naibu Meya umepelekea tumepata  posho nusu nyingine tutapewa sasa unafikili ndugu yangu maisha yataendaje bila posho wakati tunaenda kwenye mapokezi na baadae mkesha,lazima tupewe posho,"alisikika mmoja wa Diwani ambaye aliomba kutoandikwa jina lake ndani ya Blog.

Akizungumzia tukio hilo,Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi Party (DP) Chrisant Nyakitita alilaani kitendo hicho na kukiita ni utovu wa nidhamu uliofanywa na Naibu Meya akiwa kama kiongozi wa madiwani na kiongozi wa siasa kwa kuamua kufunga geti na kuchelewesha mapokezi ya mwenge kwa kile walichokiita madai ya posho na magari ya kutumia.

Alisema anakumbuka akiwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya kuratibu mapokezi ya mwenge wakiwa katika uhamasishaji kata ya Mwisenge juni 8 Naibu Meya huyo aliwatawanyisha Wananchi wasishiriki katika kikao hicho kwa kuwa suala la mwenge limepitwa na wakati.

"Nimesikitishwa sana na hatua hii,huyu Naibu Meya alikuwa mstari wa mbele kupinga mapokezi ya Mwenge kuwa yamepitwa na wakati na leo ndio anakuwa mbele kufunga geti akidai posho na magari wanayotaka sasa huu si ustarabu ni lazima tukiwa kama viongozi wa Vyama vya siasa tukimee hali hii na kila mmoja aamue kuwajibika,"alisema Nyakitita.

Katika mbio za mwenge Manispaa ya Musoma jumla ya Miradi ya Maendeleo 17 inatarajiwa kuzinduliwa yenye jumla ya shilingi milioni 904,041,293 huku Mkuu wa Wilaya musoma Jackson Msome akisema miradi hiyo imetokana na juhudi mbalimbali za Viongozi pamoja na Wananchi kwa kuamua kushiriki.Post a Comment