0

MTU mmoja Mkazi wa Kisii Nchini Kenya Josephine Bhoke Nyambani pamoja na Wegesa Ikwabe Babere Mkazi wa Nata wilayani Serengeti wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime kwa shitaka la jinai namba 344/2013 kwa kosa la hongo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi wilayani Tarime.
 
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Athumani Rugemalila,ilidaiwa na Mwendesha mashitaka wa Takukuru Mwema Mella washitakiwa hao walitenda kosa hilo juni 16 kwakumshawishi mkuu huyo wa upelelezi Hassan Maya Omary akubali kupokea pesa kiasi cha shilingi 300,000/= ili aweze kufuta kesi ya jinai namba 252/2013 iliyofunguliwa na Jeshi la polisi dhidi ya josephine Bhoke Nyambani katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime.
 
Alisema baada ya kitendo hicho cha ushawishi kinyme na kifungu cha 15 (1) (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,Mkuu huyo wa Upelelezi wa alitoa taarifa katika ofisi ya Takukuru Wilaya ya Tarime ambao walifanya mtego na kuwakamata watuhumiwa.
 
Mwema aliieleza Mahakama mnamo juni 23 siku ya jumapili washitakiwa wote kwa pamoja walikamatwa na Maafisa wa Takukuru baada ya kutoa hongo kwa Hassan Maya Omary ya shilingi elfu kumi na tano fedha ya Kenya ambayo ni sawa na shilingi laki 300,000/=.
 
Washitakiwa wote wawili wamekana mashitaka yanayowakabili na wako rumande baada ya kukosa wadhamini hadi kesi hiyo itakapotajwa tena julai 10 mwakaa huu.

Post a Comment