0
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara imeendelea kuzifatilia taasisi mbalimbali za Umma kuhusiana na matumizi mabaya ya Mamlaka huku safari hii ikiwaburuza Mahakamani waliokuwa watumishi wa Idara ya Afya katika Manispaa ya Musoma.

Watumishi waliofikishwa Mahakamani aliyekuwa Mkuu wa Idara ya afya katika Manispaa hiyo Charles Mkombachepa pamoja na aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Idara hiyo Melinda Chafora ambao wamefunguliwa shitaka la Uhujumu uchumi namba 03 ya mwaka 2013 kwa makosa ya matumizi mabaya ya Mamlaka kinyume na kifungu cha 31cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwanamba 11/2007 na kosa la kuisababishia hasara Serikali.

Hata hivyo aliyesomewa mashitaka ni mshitakiwa wa kwanza Melinda Chafora ambapo mshitakiwa pili hakuweza kufika Mahakamani na kuandikiwa hati ya mshitakiwa kufika Mahakamani juni 26 2013 ili asomewe mashitaka yake.

Mshitakiwa wa kwanza amesomewa mashitaka na Mwendesha mashitaka wa Takukuru Erick Kiwia mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mara Emanuel Ngigwana ambapo mshitakiwa amekana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana.

Mwendesha mashitaka wa Takukuru alisema kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Takukuru umebaini Melinda Chafora akiwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Afya ya Manispaa ya musoma kuanzia tarehe 15/10/2007 alitumia mamlaka yake vibaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kulikopelekea watumishi wanne ambao ajira zao zilikoma kwa kustafu na kufariki kujipatia malipo ya mishahara isiyo halali.

Alidai watu hao walijipatia kiasi cha shilingi 1,692,160.32 kwa kipindi cha mwezi julai hadi oktoba mwaka 2008 kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Alieleza kutokana na matumizi hayo mabaya ya mamlaka aliisababishia Serikali hasara ya shilingi 1,692,160.32 kinyume na aya ya 10 (1) kifungu cha 57 (1) cha jedwali la kwanza la Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002 kwa kufanya uzembe na kutokuwa makini katika kutekeleza majukumu ya kuwaondoa watumishi hao katika (payroll) za mwezi julai,agosti,septemba na okotoba mwaka 2008.

Aliongeza uchunguzi pia ulibaini mshitakiwa wa pili Charles Mkombachepa akiwa Mkuu wa Idara ya Afya katika Manispaa ya Musoma alitumia mamlaka yake vibaya wakati akitekeleza majukumu yake na kupelekea watumishi hao kujipatia mishahara hewa jumla ya shilingi 947,232.52 kwa miezi ya novemba na desemba 2008 kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007

Post a Comment