Serikali ya Marekani kupitia
Mpango wa dharula wa kupunguza makali ya VVU na Ukimwi (PEPFAR)
imeipatia Serikali ya Tanzania dola za kimarekani millioni tatu fedha
ambazo zitatumika kuwapima na kuwatibu wanawake wanaosumbuliwa na
matatizo ya saratani ya mfuko wa kizazi.
Hayo yamesemwa jana na Balozi
Leslie Rowe kutoka ofisi ya Serikali ya Marekani anayeshughulikia mambo
ya afya wakati akiongea na watu mbalimbali walioshiriki mkutano wa wake
wa Marais wa Afrika uliofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es
Salaam.
Aidha Serikali ya Marekani pia
imetoa mashine 16 za cryotherapy ambazo zitatumika kama sehemu ya
matibabu kwa ugonjwa wa saratani ya mfuko wa kizazi katika Hospitali ya
Kansa ya Ocean Road.
Balozi Rowe alisema kuwa
upatikanaji na mashine hizo utawasaidia wanawake wengi ambao
wanasumbuliwa na ugonjwa wa Kansa ya shingo ya kizazi kuweza kupata
huduma ya vipimo na matibabu mapema na haraka.
"Kutokana na maambukizi ya VVU
wanawake wengi wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa saratani
ya shingo ya kizazi na matiti kwa kushirikiana na PEPFAR tutaendelea
kuwaunga mkono utepe wa pink,utepe mwekundu kuokoa maisha ya wanawake.
Jitihada za pamoja
zinahitajika kwa kushirikiana na vikundi vya kijamii na kuimarisha
miundombinu ili kuhakikisha kuwa tunatoa vipimo na matibabu ya saratani
kwa wakati”, alisema Balozi Rowe.
Alisema kuwa uongozi wa Rais
Obama umeridhishwa na Serikali ya Tanzania kwa jinsi unavyolishughulikia
tatizo la saratani ya shingo ya kizazi na utaendelea kuwaunga mkono
wanawake na wasichana Duniani kote ikiwa ni pamoja na katanua program
mbalimbali na kutoa fedha kwa ajili ya elimu, maendeleo ya kilimo na
afya.
Akiongea na waandishi wa
Habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo Mama Kikwete aliishukuru
Taasisi ya Bush kwa kufanya mkutano huo nchini na kusema kuwa mambo
yaliyojadiliwa ni upatikanaji wa elimu kwa mwanamke, upatikanaji wa Afya
bora na kumuwezesha mwanamke kiuchumi.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa
mwanamke ni mtu muhimu sana katika jamii haijalishi ana elimu kiasi gani
yeye ni mlezi wa familia na ukimwezesha mwanamke kielimu ni ukombozi
mkubwa katika jamii kwani ni rahisi kwake kukabiliana na magonjwa
mbalimbali ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi.
“Miaka ya nyuma kutokana na
baadhi ya watu kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa wa Ukimwi
waliweza kuamini kuwa mtu akiwa na maambukizi ya ya VVU amerogwa lakini
hivi sasa baada ya watu kupata elimu wkamekuwa na uelewa mkubwa.
“Ukimwezesha mwanamke kielimu
na kiuchumi anakuwa na uhuru wa kufanya mambo yake bila ya kutegemea
msaada kutoka kwa mme wake ninachowaomba wanawake wenzangu mfanye kazi
kwa bidii kwani mwanamke akiwa na kipato cha kutosha hawezi
kudharaulika”, alisema Mama Kikwete.
Alisema kuwa zamani wanawake
wasiokuwa na kazi walikuwa wanaitwa magoli kipa ingawa walikuwa na kazi
kubwa ya kuangalia familia na jamii ikasahau kuwa wanawake ndiyo
wazalishaji mali. Pia aliwaomba wanawake wasiogope kuchangamkia fursa
zinazopatikana na wasiache kumuunga mkono mwenzao pale anapoomba nafasi
ya kupata fursa hizi kwani wakiwa pamoja wanaweza.
Katika mkutano huo pia Rais
Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa zamani wa Marekani George Bush
walitambulisha rasmi Utepe wa Pinki , Utepe mwekundu ambayo ni
alliance inayofanya kazi ya kupambana na kansa ya saratani ya mfuko wa
kizazi na saratani ya matiti katika nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara
na Amerika ya Kusini.
Tanzania ni nchi ya tatu
Barani Afrika kutambulisha Utepe wa Pinki , Utepe mwekundu alliance
nchi zingine ni Zambia na Botswana.
Mkutano huo wa siku mbili
uliomalizika jana uliandaliwa na Taasisi ya Rais mstaafu wa Marekani
George Bush na kuhudhuriwa na baadhi ya wake Wa Marais wa Afrika na Mke
wa Waziri mkuu mstaafu Wa Uingereza Cherie Blair.
Imeandikwa na Anna Nkinda – Maelezo
Post a Comment
0 comments