0
  Jumla ya Askari mia moja (100) waliofuzu usaili wa awali wa ajira ya uaskari wanatarajiwa kuanza rasmi mafunzo maalum ya mbinu za medani kwa miezi mitatu katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi kuanzia Oktoba Mosi mwaka huu. 

Askari watakaofuzu vema mafunzo hayo ndio watakaoajiriwa na shirika katika utaratibu mpya ulioanzishwa na shirika wa kuandaa mafunzo hayo kwa askari hawa waliopitia mafunzo ya uaskari katika Jeshi la Kujenga Taifa na Chuo cha Wanyamapori Pasiansi Mwanza. 

Aidha, shirika linaendelea kuchunguza na kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa wafanyakazi wanaobainika kujihusisha na vitendo vya ujangili kwa kushirikisha vyombo vya dola. Uchunguzi bado unaendelea kufanyika kwa baadhi ya wafanyakazi na utakapopatikana ushahidi wa kisheria kwa wote wanaojihusisha na mitandao ya ujangili hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa.

 Mafanikio kadhaa yameweza kufikiwa na shirika katika kukabili ujangili ambapo uimarishwaji wa doria za magari na miguu pamoja na matumizi ya mbwa katika hifadhi nchini umepunguza kwa kiwango kikubwa vitendo hivi ambapo katika kipindi cha miezi sita iliyopita ujangili uliokuwa umeshika kasi katika Hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara uliweza kudhibitiwa kwa asilimia 100 ambapo hakuna tembo aliyeuawa ndani ya hifadhi hizo tangu mwezi Februari hadi leo.

 Vile vile, Shirika limeanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujangili na matukio ya dharura (Rapid Response Team). Kikundi hiki kina Askari 40 ambao wamepewa mafunzo maalumu ya ujasiri na ukakamavu wa hali ya juu kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya ujangili katika kipindi cha miezi sita iliyopita ambapo mafunzo hayo yalifanyika katika Hifadhi ya Ruaha. Mafanikio mengine yaliyoweza kufikiwa na shirika katika muda wa miezi sita iliyopita ni pamoja na i. Ukamataji wa majangili 1,116 katika hifadhi kwa kipindi cha Aprili –Juni 2013. 

Hifadhi ya Serengeti pekee iliweza kukamata majangili 248. ii. Katika kipindi cha Aprili-Juni 2013, Askari wetu waliweza kukamata silaha za moto 85 toka kwa majangili. Silaha hizo ni pamoja na Civilian Rifle (7), muzzle loaders/magobore 60 Automatic Rifle (5) na shortgun 13. Aidha, silaha za kienyeji zipatazo 795 zilikamatwa na pia kufungua waya zinazotumika kutega wanyama 25,422. iii. Askari wa hifadhi waliweza kukamata mbao 2,245 na nguzo 1030 kwa kipindi hicho katika hifadhi zake. iv. Askari waliweza pia kukamata mifugo (ng’ombe) 6,650 waliokuwa wakichungwa ndani ya hifadhi bila vibali.

 Wenye mifugo hiyo walitozwa faini stahili. Kwa ujumla hali ya ujangili ndani ya maeneo ya hifadhi imedhibitiwa kwa kiwango kikubwa ambapo kama tulivyosema awali shirika litaendelea kuchukua hatua za kinidhamu mara moja pale itakapobainika kuhusika kwa watumishi wake katika vitendo hivi kama ambavyo limeshachukua hatua za kufukuza kazi na kuandika barua za onyo kali kwa baadhi ya maafisa wake..

 Mwisho, katika siku za usoni shirika linatarajia kubadili mfumo wake wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia na kuwa mfumo wa kamili wa kijeshi (paramilitary system) kwa watumishi wote ili kuweza kukabili kwa umakini janga la ujangili nchini. 

Imetolewa na Idara ya Uhusiano HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA 22.09.2013

Post a Comment