0
Ezekiel Kamwaga
Ezekiel Kamwaga 
Naomba, kama Ezekiel Kamwaga, kutoa maoni yangu kuhusu sakata la Katibu Mkuu wa Yanga. 
Maoni haya hayana chembe ya ushabiki ila ni maoni ya Mtanzania anayependa soka. 
Mimi sikubaliani na Ukatibu wa Yanga kupewa Mkenya. 
Na nisingekubaliana pia na Mkenya au Mganda (au raia mwingine yeyote wa kigeni) kuwa Katibu Mkuu wa Simba. 
Na hili pia halina uhusiano na ajira yangu ya Simba kwamba ninasema hivi ili kulinda kibarua changu na Katibu wangu. Siko huko. 
Niko kwenye mantiki zaidi. Nitaeleza. Ninaamini kwamba klabu hizi mbili ni miongoni mwa tunu za taifa letu la Tanzania.... 
Watu wanapenda vilabu hivi kuliko wanavyopenda kitu kingine chochote... 
Simba na Yanga ni zaidi ya CCM na CUF au CHADEMA...Unapomweka pale mgeni ni lazima kwanza upime na ujue anatoka wapi, anataka nini, katumwa na nani? 
Mtu anaweza kuamua kuvuruga amani ya nchi yetu kwa kutumia timu hizi mbili tu ! Hili ninalolisema nalifahamu vizuri... 
Pili, ni kweli kwamba hakuna MTANZANIA mwenye uwezo wa kuongoza Simba au Yanga vizuri? Nafasi hizi za kazi huwa zinatangazwa na watu wenye sifa kupeleka sifa zao? 
Au viongozi wanachagua vibaraka wao kuongoza badala ya kutafuta watu wenye uwezo ambao naamini wapo wengi tu? 
Hivi taifa hili ambalo limemtoa Julius Nyerere, Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, Nehemia Mchechu, Reginald Mengi, Patrick Ngowi na wengine wengi halina uwezo wa kutoa Katibu Mkuu tu wa Yanga au Simba? 
Tujiulize, ni wasomi na watu wangapi wenye akili zao ambao wanaweza kuja kukubali kufanya kazi Simba na Yanga kwa sasa? 
Mazingira yaliyopo sasa yanamfaa mtu mwenye heshima yake kutaka kufanya kazi Simba au Yanga? Je, Katibu Mkuu ana uwezo wa kubadili mambo na yakaenda kisasa kwenye vilabu vyetu. 
Si ni Mwalusako huyuhuyu ambaye alitangaza Ofisa Habari Mpya na akalazimishwa akanushe taarifa hiyo na baadaye ikatangazwa Ofisa Habari ni huyohuyo lakini akiwa na baraka za aliyemlazimisha Mwalusako abadili taarifa? 
Je, viongozi waliopo sasa haswa hawa watendaji, hawa wa kuajiriwa kama makatibu na wasemaji, kwenye vilabu hivi, wana nguvu ya kutosha kimamlaka kuleta mabadiliko yanayotakiwa? Tatizo ni la uraia au mfumo uliopo? 
Pia, Kenya wametuzidi nini kwenye soka yao? Huyo anayeletwa ana profile gani kwenye Soka? Alifanya nini huko alikokuwa ? Ana sifa gani ya ziada ambayo hakuna MTANZANIA mwenye nayo? 
Nasikitika sana kwamba wapo Watanzania ninaowaheshimu sana ambao wanaona kwamba wageni waje tu kuchukua ajira za wenyeji. Huu ni UTANZANIA gani? 
Huu ni UTAIFA gani tulionao. Huwezi kulinganisha Simba au Yanga na timu kama Arsenal na Man United ambazo tayari zinamilikiwa na wageni. 
HIZI MBILI NI TIMU ZETU NA ZINATAKIWA KUBAKI ZETU.... WATANZANIA WA KUFANYA HIZO KAZI WAPO. 
Kinachotakiwa ni kuboresha mazingira ya kazi. Kubadilisha mifumo ya vilabu vyetu hivi. Kwa mfumo wetu huu wa sasa, Hata umlete David Gill wa UEFA atachemsha tu. Ni maoni yangu tu...
 
CHANZO SUFIANI BLOGSPOT

Post a Comment