MVUA kubwa iliyoambatana na upepo iliyonyesha wilayani Butiama
mkoani Mara usiku wa kuamkia jana (juzi) imesababisha madhara makubwa kwa
kubomoa nyumba 66 katika kijiji cha Mwibagi na kuwaacha Wananchi bila makazi.
Kufutia tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Butiama
ilifanya ziara katika Kijiji hicho huku Mwenyekiti wa kamati hiyo Angelina Mabula
akiwahimiza Wananchi wa Kijiji hicho kuwasaidia wananchi waliopata matatizo
hayo wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya maafa hayo.
Akiwa katika kijiji hicho,Mabula alisema mvua zimeanza kwa
kasi kubwa hivyo hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kuweza kukabiliana
na athari nyingine kubwa ambazo zinaweza kutokea katika kipindi hiki cha mvua
kwa kuimaliosha nyumba ambazo zinaonekana kuwa na hufa.
Mwenyekiti wa huyo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya
Butiama pamoja na kupongeza hatua zilizochukuliwa za kusaidia wananchi
waliopata tatizo la nyumba zao kubomoka alihimiza kudumishwa kwa ushirikiano
huo wakati Serikali ikianza kufanya tathmini juu ana athari iliyotokea.
Alisema ni vyema kushirikiana kwa zile nyumba ambazo
zinaweka kukarabatika ili watu wapate makazi kwa kusaidiana baina ya Wananchi
pindi ambapo Serikali nayo inafanya jitihada za haraka kuhakikisha inatoa
msaada wa haraka kwa wahathirika.
“Serikali ipo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu
ambacho mvua iliyoambatana na upepo mkali imeharibu makazi yenu wakati
tunaendelea kufanya tathimini naomba ushirikiano uwepo hapa kijijini katika
kupeana hifadhi.
“Hili ni janga ambalo lemekuja pasipo taarifa sasa kila
mmoja alichukulie janga hili kama lake na kuweza kushirikiana katika kipindi
hiki nasi tunatambua tatizo hili na tunalichukulia hatua za haraka,”alisema
Mabula.
Mmoja wa watu
waliokumbwa na balaa la kukosa makazi katika kijiji hicho,Itembe Mtani aliiomba
Serikali kufanya tathimini ya haraka ili kuweza kuwasaidia kupata makazi kwani
familia nyingine ni duni na hazina uwezo wa kujenga nyumba hizo kwa haraka.
Alisema licha ya kukosa makazi mvua hizo pia ziliharibu
chakula chote kilichokuwa kimehifadhiwa katika nyumba zao na kwa sasa familia
hizo hazina chakula huku nyingine zikikosa pa kuishi nakuiomba Serikali
kuwaangalia kwa jicho la huruma katika kipindi hiki.
Gazeti la Habari Leo lilishuhudia baadhi ya Wananchi wenye
uwezo wakianza kujenga nyumba zao zilizobolewa huku wengine ni kama
wamerudishwa tena kwenye dimbwi la umaskini baada ya kudai hawaoni pa kuanzia.
Post a Comment
0 comments