0


WAZABUNI wa mkoani Mara wameoneshwa  kusikitishwa kwa kile walichodai mkakati wa Serikali unaolenga kuwafilisi kwa kushindwa  kulipa kiasi cha  zaidi ya shilingi bilioni 2.5  zinazotokana na madai mbalimbali  huduma zilizotolewa katika katika  taasisi mbalimbali  za Serikali mkoani humo.
 
Kiasi hicho cha fedha kinadaiwa na Wazabuni hao wa mkoa wa Mara  baada ya kutoa huduma mbalimbali  vikiwemo vyakula na mahitaji  mengine muhimu  katika  vyuo vya ualimu,vyuo vya afya,Shule za Sekondari  na Magereza.
 
Mwenyekiti wa wazabuni wa mkoa wa Mara Edward Mohere,aliwaambia waandishi wa habari mjini Musoma, kuwa kushindwa kwa Serikali kuwalipa  wazabuni hao wa ndani ni mkakati maalum  wa kuwafilisi hatua ambayo pia itachangia kuwaumiza  wakulima ambao  wamekuwa wakiuza mazao yao kwa mkopo.
 
Alisema wanasikitishwa na kauli za mara kwa mara  za Serikali ya kuwalinda wafanyabiashara  wa ndani katika kuhakikisha wanachangia kuinua uchumi na kutoa ajira kwa vijana lakini badala yake imekuwa ikikopa bidhaa,vyakula na mahitaji mengine kutoka kwa wafanyabiashara hao bila kulipa kwa kipindi kirefu sasa.
 
“Tulifikiria tuishitaki Serikali lakini tukasema  tunaamini chini ya Rais Jakaya Kikwete  tutangulize mbele uzalendo na kwamba serikali italipa deni letu hili nasi tulipe wanaotudai tena kwa riba wakiwemo wakulima lakini hadi sasa zimekuwa chenga”alisema Mohere na kuongeza.
 
“Kwa mfano juzi kuna wenzetu wemeuziwa nyumba zao na mabenki kwa kushindwa kulipa deni kwa wakati sasa wao na familia zao zinateseka hivi kweli hapa kuna haki kama si mkakati maalum wa kutufilisi”alihoji.
 
Hata hivyo mwenyekiti huyo wa Wazabuni mkoani Mara,alisema amefurahishwa na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa mkoani Iringa kuwa ni aibu kwa serikali kudaiwa na wakulima hivyo kutaka mamlaka za serikali kuondoa aibu hiyo ambayo sasa Serikali inaipata kwa kudaiwa na wazabuni.
 
“Tumetoa huduma bila vikwazo sasa kwanini kwenye kulipa kuwe na vikwazo?sisi hatuwezi kutoa rushwa ili tulipwe haki yetu hivyo ni jukumu la serikali kulipa madeni kama ilivyopata huduma kutoka kwetu”alisisitiza Mohere.
 
Mwishoni mwa mwaka jana katibu mkuu wa wizara ya elimu,afya na mambo ya ndani ya nchi kwa nyakati tofauti walikiri kudaiwa na wazabuni hao huku wakidai madeni hayo yatalipwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha (2013/4) kitu ambacho  kinadaiwa kutotekelezwa.
 
Katika kikao chao cha mwaka jana wazabuni hao walifikia azimio la kusitisha kutoa huduma kwa taasisi za Serikali na kutaka kuishitaki Serikali kabla ya kuonyesha uzalendo huo kwa kusitiza uamuzi  huo ili kuipa nafasi serikali kushughulikia madai yao.
 

Post a Comment