0
 
 
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Romani Katoriki (RC) Dayosisi ya Mara Michael Msonganzila ameiomba jamii kubadilika na kuachana na tabia mbaya ya kuwahfanyia Ukatili Wanawake na Watoto kwa kuwa kitendo cha ukatili licha ya kuwa kinamfanya muhanga kupata madhara na hata kifo lakini pia kina mdhalilisha.

Akizungumza na Wananchi wa Vijiji vya Borega na Nyiboko Kata ya Kisika Wilayani Serengeti katika maazimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili,Askofu Msonganzila alisema kuendelea kufanyika kwa vitendo vya Ukatili kwa Wanawake na Watoto kunapelekea kuendelea kuwa na familia masikini kutokana na kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi zikiwemo za kilimo.

Alisema vitendo vya Ukatili vimekuwa vikiendelea kila kukicha katika familia nyingi na kudai ili kukomesha vitendo hivyo hakuna budi kuwa na nguvu ya pamoja baina ya Serikali, Taasisi za kidini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali ili kuweza kukomesha hali hiyo ya vitendo vya Ukatili.

Askofu Msonganzila alisema katika jamii viko vitendo mbalimbali vya Ukatili vikiwemo vya kimwili,kisaikolojia na kijamii ambavyo vinafanywa na kufanya jamii kuwa dhoofu kwa mambo mengi na kukosa haki nyingi za msingi ambazo muhanga anastahili kuzipata.

Alisema kung'ang'ania mila potofu ya ukeketaji kunaendelea kuwafanya Wasichana kulazamishwa kukeketwa na kuwaacha na maumivu makali na hata kupelekea vifo kitu ambacho bila elimu ya kutosha kuendelea kutolewa mabadiliko ya kweli ya kukomesha vitendo vya ukatili haita fanikiwa.

Msonganzila alidai ili kuweka nguvu ya pamoja katika kutokomeza vitendo vya Ukatili kwenye jamii,Kanisa Katorika Jimbo la Musoma litaendeleza jitihada za kutoa elimu juu ya athari za Ukatili kwa kutumia Idara yake ya Haki na Amani pamoja na Idara ya Mipango na Maendeleo kwa kufungua matawi kila Parokia ili kutoa elimu kwa jamii.

kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma Angelina Mabula alilishukuru Kanisa Romani Katoriki pamoja na Taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha elimu madhubuti inatolewa ili kuhakikisha vitendo vya ukatili vinaondoka kwenye jamii.

Alisema ni vyema kuyatumia maazimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia kwa kufanya tathimini ya kweli ili kuondoa na kukomesha vitendo vya Ukatili vikiwemo kupiga Wanawake,Kukeketa Wasichana,kuoza wasichanawadogo,kutoa watoto wa kike shuleni na kuwaoza pamoja na kutelekeza watoto.

Mabula alisema kila mmoja analo jukumu la kupinga vitendo vya ukatili kwa nafasi yake katika jamii na kuwataka wanaofanyiwa vitendo vya ukatili kuacha kujificha na kushindwa kutoa taarifa mapema bali walitumie dawati lililopo jeshi la polisi ili wanaofanya vitendo vya ukatili waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Post a Comment