0
 
 WANAFUNZI WAKIWA NJE YA DARASA
 WIMBO WA TAIFA KABLA YA KUANZA BARAZA

 MWANASHERIA WA MANISPAA YA MUSOMA AKITOA UFAFANUZI
 MKURUGENZI WA MANISPAA YA MUSOMA AKITOA UFAFANUZI KWENYE BARAZA
 DIWANI WA KATA YA MAKOKO ALOYCE MAWAZO AKISISITIZA HATUA KUCHUKULIWA
 DIWANI WA KATA YA MWISENGE ANGELA DERRICK ALIYESIMAMA KATIKATI NI DIWANI OCHALO ALIYETUHUMIWA
 
 
IMEAMULIWA kufunguliwa taarifa polisi "RB" na Baraza la Halimashauri ya Manispaa ya Musoma juu ya uhalibifu wa majengo sita ya madarasa unaodaiwa kufanywa na Diwani wa Kata ya Kigera Gabriel Ochalo(CUF) pamoja na Kamati ya shule ya msingi Kigera A kuanza muhula wa masomo 2014.

Naibu Meya wa Halimashauri hiyo Bwire Nyamwero ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwisenge(CHADEMA) alifikia maamuzi hayo baada ya Diwani wa Kata ya Bweri Zedi Sondobhi (Chadema) kuomba Baraza lililokuwa na kikao cha kujadili na kupokea rasimu ya bajeti ya mwaka 2014-2015 kuzungumzia suala la uharibifu wa madarasa uliofanywa katika shule hiyo.

Sondobhi alisema katika muhula huu wa masomo wanafunzi wa shule ya msingi Kigera A wameshindwa kuhudhulia vipindi madarasa kwa kile kilichoonekana majengo sita ya shule hiyo kung'olewa mabati na kushindwa kuezekwa hali inayofanya wanafunzi kushindwa kusoma na kuwaaomba madiwani wakubali hoja yake na kujadili hali hiyo.

Katika majadiliano kuhusiana na hali hiyo,Mkurugenzi wa Halimashauri ya Manispaa ya Musoma Ahmed Sawa hakuwa na barua yoyote wala maagizo ya kuondolewa mabati ya shule hiyo hali iliyomfanya Naibu Meya kuomba maelezo ya kina kutoka kwa Diwani wa Kata husika juu ya uhalibifu uliofanywa kwenye shule hiyo.

Akizungumzia hali hiyo,Diwani wa Kata ya Kigera Gabriel Ochalo alilieleza Baraza hilo kusika kuwepo kwenye kikao cha Kamati ya shule kilichoamua kuondoa mabati ya majengo sita ya madarasa pamoja na kupaua kuta za majengo hayo baada ya kupokea kiasi cha shilingi milioni 3 na laki 5 kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo.

"Ni kweli nilikuwepo kwenye kikao hicho cha kamati ya shule kama mjumbe na baada ya kuona fedha hizo zimekuja na kutokana na uchakavu wa madarasa tuliamua kufanyia ukarabati lakini baada ya kuezua darasa moja yote yalitikisika na kuamua kuondoa madarasa yote na ndio maana hadi sasa kuna kukwama kunakoonekana,"alisema Ochalo.

Kufuatia majibu hayo mjadala mzito uliibuka kutoka kwa madiwani baada ya kudaiwa Diwani huyo akuzingatia taratibu na kushiriki katika shughuli ambayo imepelekea kushindwa kwa wanafunzi kuhudhuria vipindi madarasani na kuomba hatua zaidi zichukuliwe kwa wale wote waliohusika na uvunjwaji wa madarasa hayo.

Diwani wa Kata ya Makoko Aloyce Mawazo(CHADEMA) alisema hakuna sababu ya kuoneana aibu wala huruma kuhusiana na suala hilo kwa kuwa wanaoathirika ni wanafunzi na wazazi hivyo Diwani na wote waliohusika lazima wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na madarasa hayo yaezekwe mara moja ili wanafunzi waendelee na masomo.

Kutokana na mjadala huo ulichukua zaidi ya masaa mawili Naibu Meya alimuamulu Afisa Elimu Msingi kwenda kituo cha polisi kutoa taarifa juu ya uharibifu huo ili vyombo vya sheria viweze kuchukua hatua huku kamati ya maadili nayo ikitarajiwa kulizumzia suala hilo katika vikao vyake.

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi Daniel Makorere mara baada ya kutoka kituo cha polisi Musoma kati alizungumza na Waandishi wa Habari na kudai kuwa tayari ameshatoa taarifa polisi juu ya uharibifu huo na kufunguliwa taarifa ya uharibifu wa mali ya umma yenye namba MUS/RB/480/2014.

Alisema ofisi yake ilipeleka kiasi cha shilingi milioni 3 n laki 5 kwa ajili ya ukarabati wa jengo moja la darasa lakini kubomolewa kwa majengo sita hana taarifa zozote na amepokea maagizo ya Baraza hilo na kutoa taarifa polisi juu ya Diwani huyo.

Katika kikao hicho madiwa walipitisha bajeti ya shilingi bilioni 30 ikiwa ni ongezeko la asilimia 38.73 ya shilingi bilioni 21 zilizopitishwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013-2014 ikiwa ni ongezeko katika mradi wa kuboresha barabara na ongezeko la mishahara kwa watumishi wapya wa Halimashauri ya Manispaa waliopata ajira mpya kwa mwaka wa fedha 2014-2015

Post a Comment