0


JAMII ya watu wanaoishi na Ulemavu mkoani Mara wamemuomba Rais wa Jamuhuri ya Muungano Jakaya Mrisho Kikwete kuangalia upya mustakabali wa haki zao, na kwamba kama itawezekana ianzishwe Wizara inayoshughulikia walemavu bila kuchanganyikana na maswala mengine.
Hayo yalisemwa na walemavu wa ngozi(Alibino)walipokuwa wakitoa maoni wakati waliopokuwa wakichangia mada kuhusiana na mchakato wa kupata Katiba mpya na muskabari wa walemavu.

Akifungua mkutano wa kuchangia kupatikana kwa Katiba mpya,Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa ngozi mkoa wa Mara Saidi Magera alisema licha cha Rasimu ya Katiba mpya kuzungumzia haki za Walemavu bado kuna masuala mengi yahusianayo na Walemavu yaangaliwe.

Alisema bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili wanaoishi na ulemavu ambazo zinapaswa kutazamwa na Serikali ili mambo mengine ya walemavu yaweze kusonga mbele kama watu wengine.

Magere alisema Serikali ione umuhimu wa kuanzishwa kwa Wizara ambayo itakuwa ikishughulika na masuala ya walemavu ili kuweza kukabiliana moja kwa moja na changamoto zinazowakabili wanaoishi na ulemavu mbalimbali.

Mwenyekiti huyo wa Chama cha Walemavu wa Ngozi alisem akwa upande wao bado wanakabiliwa na miundombinu hafifu ya kujifunzia mashuleni ikwemo namna ya kuandika nukuu zinazotolewa ubaoni mashuleni na upatikanaji wa mafuta ya kukabiliana na jua kutokana na ngozi zao.
 

Alidai  endapo Serikali itaona umuhimu wa kuwaanzishia Wizara itakayokuwa ikiwasimamia itakuwa vyema kwa kile walichodai watakuwa na Waziri takayekuwa nao karibu kwa kuhakikisha haki za walemavu zinafanyiwa kazi.

 Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Walemavu mkoa wa Mara (Chawata) Lameck Daniel alisema kuna haja kubwa kubwa ya kuangalia changamoto zinazowakabili wenye ulemavu ili kuondokana na matatizo yanayowakabili.

Alisema katika ofisi nyingi za umma miundombinu sio rafiki kwa wenye ulemavu katika kutafuta huduma mbalimbali pamoja na mazingira ya matumizi ya vyoo katika ofisi hizo.

Lameck alisema wakati mchakato wa kupata katiba mpya ukiwa unaendelea kabla ya kupatikana kwa katiba hiyo masuala ya watu wanaoishi na ulemavu yaingizwe kwa kina kwenye katiba.
 
Alisema kuwa katika mchakato huu wa kuundwa kwa katiba mpya anaamini kuwa haki za walemavu zitathaminiwa na kwamba si kwa maandishi tu bali hata kivitendo.

Post a Comment