0
 
 
TIMU ya soka ya Kigera fc ya Manispaa ya Musoma imejitoa kushiriki ligi daraja la tatu mkoa wa Mara kwa kile ilichokieleza chama cha mpira wa miguu mkoa huo(FAM) kuipanga vituo vya mbali zaidi ya misimu minne tofauti na timu nyingine.

Barua iliyotumwa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Mara na Katibu Mkuu wa timu hiyo Thomas Maregesi ambayo nakala yake gazeti hili inayo imedai kila mwaka ratiba ambayo imekuwa ikitolewa haiitendei haki timu hiyo kwa kutokuzingatiwa kwa jografia na umbali.

Barua hiyo imeeleza kuwa licha ya timu hiyo kupangwa kituo cha Obwere Shirati wilayani Rorya katika msimu huu wa 2013-2014,chama cha soka mkoa wa Mara pia kilichelewa kutoa fumu za ushiriki wa ligi na kuziminya timu kufanya muda wa maandalizi.

Wamedai wameamua kujitoa kwenye msimu huu wa mwaka 2013-2014 kutokana na kuomba kurekebishiwa ratiba na kukataa kusikilizwa na kuongezwa kuwa katika msimu wa mwaka 2009-2010 walipangiwa kituo cha Kokaja Rorya,2010-2011 walipangiwa Kisorya Bunda na 2011-2012 walipangiwa Suguti Musoma Vijijini.

Katika hatua nyingine chama cha mpira wa miguu mkoa wa Mara(FAM) kimemteua mkufunzi wa makocha mkoa wa Mara Sindbad Madenge kuwa kocha wa timu ya mkoa wa huo inayojiandaa na mchezo wa mashindano ya Taifa dhidi ya timu ya mkoa wa Mwanza.

Katibu Mkuu wa(FAM) Mugisha Galibona alisema wanatambua uwezo wa kocha huyo hivyo wanaimani wa kukiaanda kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa machi mosi kwenye uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza kabla ya kurudiana wiki moja baadae.

Alisema wachezaji walioteuliwa wanauhakika nao kwa kuwa walichaguliwa na makocha kutoka kila Wilaya na wanauhakika wa kufanya vizuri kwenye michezo yote miwili dhidi ya timu hiyo ya mkoa wa Mwanza.

Post a Comment