KANENA RAIS KUHUSU KATIBA YA TANZANIA
Rais Jakaya Kikwete, amesema kero za Muungano zinaweza kutatuliwa bila kuwa na serikali tatu.
Akizindua rasmi Bunge Maalumu la Katiba jana mjini Dodoma alisema muundo wa serikali tatu hauwezi kuwepo bila kuwa na rasilimali zake.
Aliwatahadharisha wajumbe wa bunge hilo kuwa makini kabla ya kuchukua uamuzi ambao unaweza kuisababisha nchi kuingia kwenye hatari.
"Hii serikali isiyo na uwezo, tegemezi ambayo haina dhamana, itakuwa inasimamiwa na wanajeshi ambao wakishindwa kulipwa mishahara baada ya miaka mitano wakavua magwanda na kupindua nchi," alionya.
Hata hivyo, alisema: "watakachoamua Watanzania ni hicho hicho, wakiamua mbili tutakwenda huko huko, wakiamua tatu, tutakwenda, lakini kweli serikali hii itasimama?" alihoji na kuongeza kuwa suala la mfumo wa serikali tatu si jambo dogo ni lazima watu wawe makini kuamua.
Akireja hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema hata takwimu zilizotolewa kwenye rasimu hiyo haizionyeshi ukweli wa wananchi kutaka serikali hizo.
"Hata Tume hawana majibu hayo, mkishaanza kujenga hisia za kitaifa na Utanganyika ikajengeka, mtaleta matatizo," alionya.
“Sisi ni viongozi hatuna budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa tusije tukaona watu wanafukuzana na mali zao kuporwa na matokeo yake ni muungano kufa.
Aliwataka wajumbe kusoma vizuri na kuelewa kila kilichoandikwa ili kila mtu aweze kuchukua uamuzi wake na si kuambiwa na kuonyesha wasiwasi kuwa kuna hatari ya nchi kupoteza kila kitu walichokijenga miaka 50 iliyopita .
"Nawapongeza kwa bahati ya aina yake mliyoipata ya kutunga katiba ya Tanzania, mkifanikiwa kuipatia katiba ya Tanzania majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu," alisema.
Aliwaambia ni matumaini ya Watanzania kuwa watatunga katiba inayokubalika na wengi, inayotekelezeka na inayoimarisha Muungano, ushirikiano na mshikamano, licha ya tofuati zilizopo na kuandika katiba itakayojali mfumo wa kidemokrasia na inayowezesha kukuza uchumi wa nchi.
Alionya kuwa wapo baadhi walioamini kuwa katiba mpya itawapa ushindi dhidi ya CCM, walifikiri ushindi wa CCM upo katika katiba hiyo.
Akichambua rasimu hiyo alisema imependekeza mambo mengi, kati ya pendekezo la msingi la Tume ni kuwa na serikali ya tatu ambayo kimsingi ni majukumu ya serikali ya nchi washirika.
Alisema kuna mambo muhimu yanayohitaji kuingizwa katika mfumo wa serikali tatu, baadhi yao yakiwa ni ulinzi na usalama, uhamiaji, sarafu, ushuru wa bidhaa na mapato ya kodi yatokanayo na jamhuri ya muungano.
“Kilimo kimeingia wapi katika rasimu, yakiachwa hayo siku yakwanza tu yataleta mgongano, lazima wajumbe msome na myaelewe,” alisema na kuongeza “Mkichagua mfumo wa serikali tatu lazima hayo yatashindwa kutekelezeka.”
Alisema kama wananchi wataamua kuendelea kuwa na mfumo wa serikali mbili mambo haya yanatekeleza bila taabu
Alisema katika rasimu ya katiba, utumishi wa serikali halikuelezwa kama jambo la Muungano, “sasa wale ni wanani?” Msipoyatazama kwa makini...siku mnamaliza tu inayofuata watu watalalamika.”
Aliwaambia wajumbe kuwa anaamini wakiisoma rasimu kwa makini wanaweza kugundua na mengine. “Naomba mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na manufaa yake.“Sifa ya katiba ni hii haitakiwi iwe na upungufu.”
“Kwanza muwe watulivu mnapojadili suala hili, mkilijadili kwa jazba, wenye hasira hawajengi, hawatengenezi jambo vizuri, epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi, kwani uamuzi usio sahihi unaweza kusababisha hasara na nchi kujaa migogoro.
Alisema mijadala ya kutaka serikali tatu si jambo jipya, ilikuwepo wakati wa kuunganisha nchi mbili, ulikuwa kiini cha kuchafuka hali ya hewa ya kisiasa, Zanzibar .
“Nafurahi mnalizungumza, hili mlijadili mlimalize tufanye mambo mengine. Waasisi wa taifa letu Mwalimu Nyerere na Abeid Karume, waliamua muundo wa serikali mbili.” Alisema.
“Muuundo ambao hauwezi kuimeza Zanzibar na muunda ambao unaupunguzia mzigo serikali ya Muungano. Mnapouzungumzia kuujadili hamuwezi kuwaepuka waasisi hawa.
Alisema tume imependekeza muundo huo ndiyo matakwa ya wananchi wengi, kote Zanzibar na Bara, sababu ya pili muundo huu unatoa jawabu la matatizo mengi ya pande mbili.
Wapo wanaosema kweli Tume imesema muundo wa serikali tatu ndio unaokubalika, lakini takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo.
"Mi nasema wanayosema, kwa sababu hatimaye uamuzi ni wenu nyie, wanasema wananchi waliotoa maoni kwa mdomo.. 47,820 ndiyo waliokerwa na muundo wa muungano.Ingethibisha kwenye uwingi wa waliotoa hoja.... nawaachia nyie mjadili.”
Sababu ya pili inayotoa tume ni kwamba inajibu changamoto nyingi za serikali pili mipaka ya muungano haijaanishwa vizuri kwenye rasmu, ipi inaishia wapi na mgawanyo wa mapato.
Aliwaambia , “mkijadili muundo wa serikali tatu haya myatambue na mtafutie majibu muafaka wa changamoto hizi. Kupanga ni kuchagua, ” hata hivyo, aliipongeza Tume ya Warioba kwa kufanyakazi kitalaamu na kwa uaminifu.
Alitaja kero za serikali mbili kuwa Tume ya pamoja, Mgawanyo wa mapato, ushirikiano wa zanizbar na taasisi za nje. ajira za watumishi na usajili wa vyombo vya moto.
Serikali za nchi mbili ndio zilizoingia katika mkataba wa mabadiliko haya ya katiba ili kushughulikia changamoto hizo zinazojitokeza.
"Mimi naishi kwa matumaini na kwa vile tunayo dhamira njema haya yaliyo kwenye migongano ya katiba, yataisha."Tukishakata tamaa kwenye muungano huu hakuna kitakachowezekana.
“Lazima tujipe matumaini kwamba yapo tunayoweza kuyafanya, mimi ninaamini na hata wengine wengi wanaamini dhamira hiyo tunayo.”
Hatuna dhamira ya kisiasa ya kupunguza kile kinachopunguzika. Kila kilichoongezeka katika muungano kulikuwa na sababu zinazokubalika na pande mbili za muungano.
Aliwataka wajumbe kuchunga lugha zao na matendo yao ili kutowafanya Watanzania kukata tamaa, hakuna haja ya kutishana na kukingiana ngumi.
CHANZO IPPMEDIA
Post a Comment
0 comments