0
 AFISA WA TAKUKURU MKOA WA MARA SHANI RAMADHANI AKIZUNGUMZA KWENYE MKUTANO WA WADAU WA ELIMU WILAYA YA BUTIAMA
TAASISI ya Kuzui na Kupambana na Rushwa mkoani Mara(TAKUKURU) imewataka waratibu wa elimu,walimu wakuu pamoja na wananchi kuwatolea taarifa walimu ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao kwa kuhudhuria vipindi madarasani na kwenda kufanya shughuli nyingine na kupelekea wanafunzi kufanya vibaya madarasani na kwenye mitihani.

Kauli hiyo ilitolewa na afisa wa Takukuru Kitengo cha Elimu kwa Umma Shani Ramadhani katika mkutano wa wadau wa elimu Halimashauri ya Wilaya ya Butiama waliokuwa wakijadili namna ya kuinua elimu kwenye Wilaya hiyo kutokana na kufanya vibaya mitihani ya mwisho muhula wa 2013 na kuwa Wilaya ya mwisho mkoani Mara.

Alisema kitendo cha walimu kushindwa kuhudhulia vipindi madarasani na kwenda kufanya shughuli zao mbalimbali zikiwemo uendeshaji wa pikipiki(bodaboda)na kujiingiza katika ushabiki wa vyama vya siasa ni kinyume cha taratibu na maadili ya kazi aliyoajiliwa nayo hivyo wanaohusika na uangalizi wa walimu pamoja na wananchi wanapaswa kuwatolea taarifa Takukuru ili wafatiliwe na kuchunguzwa.

Shani alisema kwa mujibu wa sheria ya kupambana na Rushwa kifungu cha 96 ya sheria hiyo ya mwaka 2007 inamuingiza hatiani mwalimu ambaye hatawajibika kwenye nafasi yake na hivyo kupelekea kujipatia manufaa na kuwataka walimu kuhakikisha wanawajibika kwenye nafasi zao ili kuweza kuwasaidia wanafunzi waweze kufanya vizuri madarasani na kwenye mitihani yao.

Ofisa huyo wa Takukuru alisema licha ya kutolewa sababu nyingi ya kushuka kwa kiwango cha elimu katika Wilaya hiyo suala pia la walimu kutohudhulia kwenye vipindi vyao madarasani kunapelekea ufaulu mbaya wa wanafunzi na kuzalisha kizazi ambacho kinakosa elimu na kuwa janga kubwa kwa Taifa.

Alisema pia licha ya sheria ya kupambana na Rushwa kumbana mwalimu ambaye anashindwa kutimiza wajibu wake pia viongozi wakiwemo waratibu wa elimu,walimu wakuu pamoja na wakuu wa idara ambao watashindwa kuwatolea taarifa walimu wanaoshindwa kuhudhulia vipindi madarasani pia sheria hiyo kifungu cha 31 cha sheria ya kupambana na Rushwa Sura ya 11 ya mwaka 2007 inambana kiongozi kutokana na matumizi mabaya ya mamlaka hivyo asipotoa taarifa atachukuliwa hatua na Takukuru.

Akizungumza katika mkutano huo uliowahusisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo walimu na mashirika binafsi,Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Musoma Denis Ekwabi aliwaomba Takukuru pia kuwachunguza baadhi ya madiwani ambao wamekuwa wakiomba Rushwa kwa walimu ili waweze kusaini fomu za kutolea pesa benki kwa ajili ya maendeleo ya shule.

Alisema wapo wanasiasa ambao kwa nafasi ya kisiasa wanachangia kudidimiza elimu kwa kuwabana walimu kwenye maeneo yao kutokana na nafasi hiyo huku wengine wakishinikiza kupewa Rushwa ili waweze kusaini fomu za kuidhinisha kutoa pesa benki hivyo kuwaomba maafisa wa Takukuru kuwachunguza wanasiasa hao.

Baadhi ya walimu waliohudhulia mkutano huo walisema licha ya kila mmoja kuwanyooshea kidole kutokana na kushuka kwa kiwango cha elimu kwenye Halimashauri ya Wilaya ya Butiama bado walimu wanazo changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo madeni wanayodai Serikali pamoja na michango ya kuchangia nyumba za walimu kitu ambacho kinawafanya walimu kuona njia mbadla ya kujiongezea kipato.

Post a Comment