0
 
MWAKA jana wakati wa maazimisho ya miaka 14 tangu kutokea kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere niliandika makala nikiangazia shule ya msingi Mwisenge aliyosoma mtu ambae kila mwaka imewekwa siku ya kumkumbuka kutokana na mazuri aliyofanya kwenye taifa hili.
 
Nilizungumzia changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwemo upungufu wa matundu ya vyoo wanavyotumia wanafunzi wanaosoma kwenye shle hiyo na kutoa angalizo itakapofika kumbukumbu ya miaka 15 kama ilivyofika hii leo kusiwepo na maandishi ya wanafunzi kukosa mahala pa kujisaidia.
 
Wakati wa kumbukumbu hiyo mwaka jana,mwalimu Mkuu wa shule hiyo Redigunda Tairo alidai licha ya shule hiyo kuwa na historia kubwa alidai changamoto za shule  kutokuendana na yale yaliyofanywa na muasisi wa taifa hili ambapo alidai licha ya kero kubwa ya upungufu wa matundu ya choo lakini bado walimu wanaishi kwenye nyumba chakavu.
 
Ikiwa tunaanzimisha mika 15 hii leo tangu kifo cha muasisi wa taifa hili na nikiwa bado natamani kuiona siku moja shule ya msingi Mwisenge ikiwa sehemu muhimu ya historia tunapokumbuka mengi yaliyofanywa nae bado ntaendelea kuiandikia ili siku moja kile nnachokitamani kiweze kuwafanikiwa.
 
Nnapoandika makala hii ya mika 15 baada ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere sina budi kuanza kulishukuru Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)kwa uwamuzi wa kuiona changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo kwenye shule hiyo na kuamua kujenga jengo la kisasa lenye matundu 14 kwaajili ya wanafunzi wa kike na kiume.
 
Ni jambo ambalo naliona lilifanywa na moyo wa kizalendo na shirika hilo kwa muamua kutumia kiasi cha shilingi milioni 14 kupunguza changamoto ya upungufu huo na leo mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mwisenge anakili msaada huo kuwapunguzia wanafunzi hadha ya wengine kurudi nyumbani kwaajili ya kupata huduma ya choo.
 
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo  ambayo licha ya kusomwa na Mwalimu Nyerere wapo viongozi wengine wengi waliosoma shuleni hapo akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba anakili kuwepo na changamoto nyingine nyingi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi ili yale maswali mengi juu ya shule hii yasiendelee kuwepo.
 
Mwalimu Redigunda Tairo anadai licha ya Shirika la Nyumba kutoa msaada wa ujenzi wa matundu ya vyoo pamoja na majengo yake bado kuna upungufu kutokana na wingi wa wanafunzi waliopo kwenye shule hiyo ambayo kwa sasa imeganywa A na B na kudai bado kuna uhitaji wa matundu zaidi ili kuondoa upungufu uliopo.
 
“Shule nzima kwa sasa ina idadi ya wanafunzi 808,idadi hii ni kubwa na ikumbukwe pia shle hii ina kitengo cha wanafunzi walemavu hivyo huduma za vyoo pia zinatakiwa kuwatazama na watoto wanaoishi na ulemavu kwa kujengwa kwa vyoo vyenye miundombinu rafiki.
 
“Tunalishukuru shirika la nyumba kwa ule msaada wao walioutoa mwaka jana na kupunguza upungufu mkubwa tuliokuwa nao katika siku za nyuma lakini bado tunawaomba wadau wengine kuitazama shule hii kwa jicho la pekee na hasa kutokana na kumbukumbu yake,alisema Tairo.
 
Anasema licha ya changamoto hiyo ya matundu ya vyoo kwa wanafunzi,bado pia walimu wa shule hiyo ambao pia uhusika kufundisha vitengo vya wanafunzi wenye ulemavu hawana nyumba za kuishi shuleni hapo ili kuweza kuwahudumia kwa ukaribu hasa wanafunzi wenye ulemavu ambao wanaishi shuleni hapo.
 
Tairo anadai majengo ya nyumba za walimu yaliyopo shuleni hapo ni chakavu sana na kiomba serikali pamoja na wadau wengine kujitoa kiusaidia shule hiyo ili pale inapokuwa inaanzimishwa kumbukumbu ya mwalimu Nyerere shule hiyo pia iwe sehemu ya kumbukumbu sahihi.
 
“Baadhi ya majengo hali yake ni nzuri kutokana na Serikali kuamua kuyakarabati ili kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini mengine bado hayajakarabatiwa ni chakavu na nyumba wanazoishi walimu ni mbovu na haziendani na hadhi ya jina la shule hii.
 
“Ile nyumba unayoiona ndio aliyokuwa anaishi Mwalimu aliyekuwa anamfundisha muasisi wa Taifa hili pamoja na viongozi wengine waliopata kusoma kwenye shule hii ni budi viongozi waliopata kupitia hapa na wadau wengine waienzi shule hii,”.
 
Haya ni maneno niliyomnukuu mwalimu Tairo kwenye makala niliyoandika mwaka jana katika kumbukumbu ya miaka 14 baada ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere lakini leo nnapoandika kumbukumbu ya miaka 15 majengo ya nyumba za walimu bado ni chakavu na kuwafanya walimu kwenda kupanga mbali na shule.
 
Kaimu Afisa Elimu ya Msingi Manispaa ya Musoma Machera anasema Serikali imekuwa ikitenga fedha katika kuifanyia maboresho shule hiyo ili kuifanya kuwa na kumbukumbu nzuri kwa kurekebisha majengo bila bila kuondoa kumbukumbu ambazo zipo tangu Mwalimu Nyerere akisoma shuleni hapo.
 
Anasema kwa sasa Idara ya Elimu kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha shule hiyo inazungushiwa uzio ili kuwafanya wanafunzi wenye ulemavu kusomea na kuishi sehemu salama bila kubughudhiwa.


“Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inamgusa kila mmoja,Idara ya Elimu ya Msingi Manispaa ya Musoma inamuomba kila mmoja anayeguswa na shule hii pamoja na kumuenzi Mwalimu tunamkaribisha kuja kusaidia kuboresha shule hii,”alisema Machera.
 
 

Mwalimu wa Mwalimu Nyerere Marehemu James Irenge kabla ya mauti yake alikuwa akisema Mwalimu Nyerere ni mtu muhimu katika taifa hili na kila mmoja anapswa anapomuenzi aenziwe kwa dhati.

 “Alikuwa mwanafunzi wa ajabu sana.Alikuwa na upeo wa juu. Alisoma madarasa manne kwa miaka mitatu. Mwaka 1937, alihamia shule nyingine mkoani Tabora kuendelea na darasa la tano,”anasema mwalimu huyo wa Baba wa Taifa 
 
“Alikuwa kijana mwenye kusikiliza mafundisho ya darasani au kutoka kwa mtu yeyote mwenye akili. Alikuwa na akili za kuzaliwa,” anasisitiza mzee huyu, ambaye ameandika mswada unaosema ‘Maisha na Sifa za Viongozi wa Tanzania Kabla na Baada ya Uhuru’, lakini kutokana na kukosa pesa, ameshindwa kuuchapisha kuwa kitabu.sehemu ya nukuu za mwalimu wa mwalimu nyerere
 
Nilisema kwenye makala iliyopita Serikali na wadau mbalimbali ambao kila uchao tunapaza sauti za kusema mazuri yaliyofanywa na Mwalimu Nyerere tukiamua kumuenzi kwa vitendo tutafanya lakini tukiamua tutaacha.
 
Kule kutembea umbali wa kilometa 37 kutoka Kijiji cha Mwitongo Butiama hadi shule ya msingi kutafuta elimu kwa muasisi wa taifa hilo kuone suala la elimu ni suala la msingi na shule ya msingi Mwisenge kufanywe kama sehemu sahihi ya kumbukumbu ya elimu ya msingi ya muasisi huyu.
 
Nirudie tena maneno haya,hivi ni kweli tunapofanya kumbukumbu hii tunashindwa kuitembelea shule ya Mwisenge na kujua changamoto zake ili tusiwe na mambo mengi ya kuandika tukiwa tunamkumbuka muasisi wa taifa hili?.
 
Majibu ya swali hili ni rahisi tunajionyesha tupo karibu katika kumkumbuka ya Mwalimu kumbe ni unafiki huku tukiona wanafunzi wanaosoma kwenye shule aliyoma wakikosa sehemu ya kujisaidia,maji na wengine wakikaa chini.


 
 

Post a Comment