WAWILI WAFARIKI DUNIA KWA KULA UYOGA
Na Thomas Dominick,
Nanyumbu
WATU wawili wa familia moja wafariki dunia katika kijiji cha
Masyalele, Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara na wengine wanne walazwa
akiwemo mtoto wa miaka mitatu katika kituo cha afya cha Mangaka baada
ya kula uyoga unaosadikiwa una sumu.
Tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki baada ya mume na mke kufikishwa
katika kituo hicho cha afya Januari 24 mwaka huu ambapo walilazwa
lakini baada ya muda mfupi walifariki.
Akizungumza na Mwandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu Mganga
Mkuu wa Wilaya hiyo, Salvatory Chinguile alisema kuwa marehemu hao
baada ya kufikisha katika kituo hicho hawakusema ukweli kama wamekula
uyoga na baada ya kufanyiwa uchunguzi walikutwa wana malaria kali.
"Baada ya kufika katika kituo cha afya hawakusema kama wamekula uyoga
na ndipo tuliwafanyia uchunguzi na kukuta wana malaria kali na
kuwaanzishia matibabu lakini walifariki wakati tukiendelea na
matibabu,"alisema Chinguile.
Dokta Chinguile aliwataja marehemu hao kuwa ni Hasani Mtumbele (68) na
mkewe Zena Ibrahimu (55) pia aliwataja waliolazwa ni Shamila Faina
(19), Mohamed Milinje (69), Maimuna Bakari (29) na Keshneti Kazumari
(3).
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga amewataka wananchi wa wilaya
hiyo kuacha kula uyoga ili kuepukana na madhara ambayo yanaweza
kujitokeza pamoja na kusababisha vifo.
"Nawaomba na nashauri wananchi wote waache kula uyoga kwa sasa kwani
wananweza kupata madhara makubwa hata kusababisha vifo kutokana na
uyoga mwingi kuwa na sumu,"alisema Kiswaga.
Pia alisema kuwa wilaya imepeleka timu ya madaktari watatu kwa ajili
ya kuwafanyia uchunguzi wananchi wa eneo hilo ambao walikula uyoga
tangu zilipoanza mvua.
Post a Comment
0 comments