0
MAZOEZI YA TIMU YA POLISI MARA YAKIENDELEA KWENYE UWANJA WA KUMBUKUMBU YA KARUME TAYARI KWA MCHEZO WA LIGI DARAJA LA KWANZA DHIDI YA RHINO YA TABORA
KIUNGO WA POLISI MARA SAID HAMZA CHEPE AKIFATILIA MAZOEZI HUKU AKIPATA BURUDANI BAADA KUWA NA MAUMIVU YA PAJA
Na Shomari Binda
         Musoma,

Timu ya soka ya maafande wa Polisi Mara kesho itawapasa kujiuliza ni makosa gani yaliyopelekea kufungwa katika michezo yao miwili ya ligi daraja la kwanza katika uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na Kambarage Shinyanga mbele ya mashabiki wake pale itakapoikaribisha timu ya Rhino ya Tabora katika mchezo wake wa tatu utakaopigwa katika dimba la kumbukumbu ya karume mjini Musoma.

Mashabiki wa timu hiyo ambao wanashauku ya kuiona ligi kuu msimu ujao,wameshitushwa na vipigo katika michezo hiyo miwili na sasa wana hamu ya kuona ikichomoza na ushindi katika mchezo huo wa tatu ili kuwawekea matumaini kama lengo la kupanda ligi kuu msimu ujao litafanikiwa.

Akizungumza na blogu hii katika mazoezi ya timu hiyo, kocha mkuu wa timu ya Polisi Mara Hafidh Salim alisema wachezaji wake walipoteza michezo miwili ya utangulizi kutokana na kutojiamini lakini suala hilo amekwisha kulifanyia kazi na anaamini watachomoza na ushindi katika michezo inayofuatia.

Alisema wacheza wote wapo katika hali nzuri tayari kwa mchezo huo tofauti na mchezaji wake Abdara Abdara aliyepewa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Mwadui ya Shinyanga katika uwanja wa Kambarage mjini humo.

Hafidh alidai kuwa anatambua kile ambacho mashabiki wa soka Mkoani Mara wanachokihitaji na atahakikisha anawajenga kisaikolojia wachezaji wake ili waweze kufanya vizuri katika mchezo huo muhimu katika kujiweka katika mazingira mazuri.

Naye Mwenyekiti wa timu hiyo Alon Mihayo alisema upande wa uongozi imewatekelezea wachezaji na benchi la ufundi kila kinachohitajika kilichobaki ni kuwapa raha mashabiki wa soka katika Mkoa wa Mara ambao wameonekana kuwa na hamasa kubwa katika mchezo wa soka.

Mihayo katika kutoa hamasa katika mchezo huo amewaomba mashabiki na wadau wa timu hiyo kutoka maeneo mbalimbali kuja kuongeza nguvu ya ushangiliaji ili kuwapo nguvu wachezaji waweze kufanya vizuri uwanjani na kuibuka na ushindi katika mchezo wa leo dhidi ya wanajeshi wa Rhino kutoka Tabora.

Katika mchezo wa kwanza Polisi Mara ilikubali kichapo cha mabao 3-2  kutoka kwa mabingwa wa zamani wa Tanzania timu Ya Pamba ya Mwanza kabla ya kusafiri hadi Mkoani Shinyanga na kubugizwa mabao 3-0 toka kwa Mwadui.

Tayari timu ya Rhino imeingia Mjini Musoma tangu siku ya jumatatu tayari kwa mchezo ikitokea Mkoani Mwanza baada ya kulazimishwa sare na Pamba siku ya jumapili na imekuwa ikijifua katika viwanja vya 27kj Makoko chini ya uangalizi mkali

Post a Comment