0
SEHEMU YA JUU YA KIVUKO CHA MV.MUSOMA 
Na Shomari Binda
           Musoma,

BAADHI ya watu wasiofahamika ambao bado wanaendelea kufatiliwa na vyombo vya sheria wamedaiwa kupanga mbinu chafu za kuharibu mashine za kivuko kinachotoa huduma za usafiri kati ya Manispaa ya Musoma na Kinesi Wilayani Rorya kwa madai kuwa baada ya kuja kwa kivuko hicho wameshindwa kufanya biashara na kupaki vyombo vyao vya usafiri.

Akizungumza na brogu hii Ofisini kwake,Meneja Wakala wa Ufundi (TEMESA) Mkoani Mara Eng;Reuben Mateso alisema zipo taarifa ambazo zimetolewa Ofisini kwake na Raia wema kuwa wapo baadhi ya watu ambao hawakupendezwa na kuja kwa kivuko hicho kutokana na maslahi yao binafsi hivyo wanapanga mipango mibaya ya kukifanyia hujuma kishindwe kufanya safari zake.

Alisema watu hao wamekuwa wakiweka mitego yao ya kuvulia samaki katika njia inazopita kivuko hicho wakiwa na lengo la kuharibu injini na kushindwa kufanya safari zake ili wao waendelee na shughuli zao za usafirishaji walizokuwa wakizianya awali kabla ya Serikali kukileta kivuko hicho kwa ajili ya kutoa huduma kwa Wananchi.

Mateso alisema licha ya sheria kuzuia kutega katika maeneo ya njia za kivuko na kutangazwa kwa matangazo hayo katika maeneo mbalimbali bado kuna watu wanaondelea na shughuli za utegaji kwa siri hasa nyakati za usiku hivyo kutaka kukwamisha huduma ya kivuko hicho ambacho kimekuwa mkombozi kwa Wananchi walio wengi.

"Naamini ni watu wachache wanaounda mbinu hizi chafu kwa masrahi yao binafsi kwa sababu Wananchi walio wengi wamefurahi ujio wa kivuko hiki kwa kurahisisha shughuli zao mbalimbali pamoja na kiasi kidogo cha nauli ambacho kimepangwa na Serikali tofauti na nauli ambayo walikuwa wakitozwa kabla ya ujio wake,"alisema Mateso.

Alisema Wananchi wanaoona umuhimu wa kivuko hicho ndio wamekuwa wakiwapa taarifa za kuundwa kwa hujuma za kukikwamisha kivuko ambapo tayari wamesha wasiliana na Mamlaka zinazo husika ikiwa ni pamoja na kufikisha taarifa kwa Wakala Mkuu (TEMESA) Makao makuu Jijini Dar es salaam ili hatua mbalimbali za kiusalama ziweze kuchukuliwa.

"Hivi karibuni mitego iliingia katika moja ya mashine kati ya mbili ya kivuko kikiwa njiani hali iliyopelekea kutembea na mashine moja hadi Kinesi na hii ni hatari lazima hatua za haraka ziweze kuchukuliwa maana matokeo ya hujuma hizi za watu wachache kwa maslahi yao binafsi ni mbaya kwa walio wengi,"aliongeza Mateso.

Alidai hadi sasa wamekwisha kukamata mitego mengi katika njia za kivuko hicho huku wahusika wake wakiwa hawajafahamika na jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi zinafanywa ili kuwabaini wale wote wanaohusika na hujuma hizo ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Meneja huyo wa Temesa Mkoani Mara alisema Serikali ina nia njema za kuleta kivuko hicho kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa Wananchi hivyo kuomba kuendelea kutolewa kwa ushirikiano na taarifa kutoka kwa Wananchi juu ya watu ambao kwa masrahi yao binafsi wanataka kukifanyia hujuma kivuko hicho.

Katika hatua nyingine Meneja wa Temesa Mkoani Mara Eng;Reuben Mateso ameshangazwa na kitendo cha Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi kavu (Sumatra) kwa kukaa na Chama cha Wasafirishaji wa mizigo na abiria Mkoani Mara na kuruhusu boti binafsi kutumia njia za feri ambapo ni kinyume cha sheria.

Alisema popote kwenye feri ya Serikali hairuhusiwi kutumiwa na vyombo vingine na kulalamika kushindwa kushirikishwa katika kikao hicho ambapo kama angeshiriki asingekabliana na suala hilo kwa kuwa ni kinyume cha sheria na tayari ameshalitolea taarifa kwa Wakala Mkuu na vyombo vingine vinavyohusika.

Post a Comment