0
Mbunge atangaza vita na Nyani waharibifu

          -Mwananchi atakayeua nyani na kumpelekea mkia kulipwa elfu kumi

    Na Shomari Binda,
         Bunda

Mbunge wa Jimbo la Kibara Kangi Lugora (CCM) ametangaza vita na Nyani ambao amedai wamekuwa wakiharibu mazao ya Wananchi mashambani na wengine kuwadhuru watu katika maeneo yao ya makazi na kupelekea kukwamisha shughuli za kiuchumi zinazofanywa na Wananchi katika Jimbo hilo.

Akizungumza na BLOGU HII Mjini Bunda Kangi alisema tayari walishatoa taarifa Serikalini kupitia Wizara ya Mali Asili na Utalii kuhusiana na uharibifu unaofanywa na Nyani hao lakini wamekuwa kimya bila kuchukua hatua zinazostahili hivyo amaeamua kuwahamasisha Wananchi katika Jimbo lake kuhakikisha wanawaangaamiza Nyani wote katika maeneo yao.

Alisema nyani hao wamekuwa wakifanya uharibifu mkubwa ambao wameshindwa kuuvulia wakati walishatoa taarifa katika sehemu zinazohusika na kukaliwa kimya hivyo wameamua kwa nguvu zao kuhakikisha wanapambana na nyani hao na kuwaondoa kabisa katika maeneo yao.

Mbunge huyo alisema amewaajili watu watano ambao wanatumia siraha za bunduki na kijadi kuhakikisha popote wanakutana na nyani  kuwaua ili wasiendelee kuharibu mazao ya Wananchi na kuwadhuru binadamu kwa kuwa Serikali imeshindwa kulichukulia hatua suala hilo.

Alisema licha ya kuwaajili watu hao pia amewatangazia ajira Wananchi wa Jimbo hilo kwa yeyote atakaye ua nyani na kisha kumpelekea mkia atapewa shilingi elfu kumi papo hapo kwa kuwa amewaweka mawakala ambao wanatumia stakabadhi ambazo zimeandaliwa kwa kazi hiyo ya kuwalipa Wananchi.

"Hatuwezi kuendelea kukubaliana na hali hii ya kuharibiwa mazao yetu huku Serikali imekaa kimya tutawaua nyani wote kwa kuwa hawana faida kwetu na nimeshaandaa fedha za kutosha ambazo kila Mwananchi atakayefanya kazi hiyo atapata malipo yake,"alisema Kangi.

Alisema nyani hao wamekithiri sana katika milima ya Lagata,Ilamba na Kitengere ambapo amedai huko kote amewaweka mawakala ambao watahakikisha kila Mwananchi atakayepeleka mkia wa nyani anapata malipo yake papo hapo pasipo usumbufu.

"Kwanza nyani hawa sio utalii kwetu na hakuna mtu yeyote anayekuja hapa kufanya utalii wa kuangalia nyani na kama Serikali ingeona wanafaa kwa utalii wangesikiliza vilio vya Wananchi kutokana na adha wanayoipata ya kuharibiwa mazao yao na kuwadhuru Wananchi,"alisema Mbunge huyo. 

Mbunge Kangi aliongeza kuwa licha ya uharibifu wa nyani hao lakini pia kumekuwepo na matukio ya Wananchi kudhuliwa na Mamba pamoja na Viboko katika Ziwa Victoria ambapo pia wameanzisha vita ya kuhakikisha wanawawinda mamba pamoja na viboko na kuwaua.

Alisema hadi sasa watu wanne wameuwawa na mamba pamoja na viboko huku Serikali ikikaa kimya hivyo wao wameamua kuanzisha mapambano ambayo yatawaangamiza mamba na vibiko wote ambao wamekuwa wakiwadhuru Wananchi. 

Post a Comment