Bradford
City imewashangaza wengi kwa kuilaza timu inayoshiriki katika ligi kuu
ya Premier kwa magoli 3-1, katika mechi ya raundi ya kwanza ya kuwania
kombe la ligi.
Timu hiyo inayoshiriki ligi daraja ya pili, inashikilia nafasi sitini nyuma ya Aston Villa katika orodha ya timu bora nchini Uingereza.
Aston Villa sasa itahitaji kuilaza Bradford City kwa zaidi ya magoli mawili kwa bila katika mechi ya raundi ya pili ili kufuzu kwa fainali hizo.
Kufikia wakati wa mapunziko, Bradford ilikuwa ikiongoza kwa bao moja kwa bila lililofungwa na Nahki Wells.
Kipa wa Bradford Matt Duke, alizuia makombora makali kutoka kwa washambulizi wa Aston Villa waliokuwa wakiongozwa na Christian Benteke.
Baada ya kipindi cha pili kuanza, wenyeji waliendeleza mashambulio yao na juhudi zao zilizaa matunda pale Rory McArdle alipoifungia Bradford bao lake la pili dakika kumi na tatu kabla ya mechi hiyo kumalizika.
Wachezaji wa Villa hawakufa moyo na waliendeleza mashambulio yao na kupata bao lao la kwanza kupitia kwa mchezaji Andreas Weimann.
Matumaini ya Villa ya kukomba bao la pili, yalizimwa kabisa dakika chache baadaye na Carl McHugh ambaye aliifungia Bradford bao lake la tatu kwa kichwa, baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Gary Jones.
Ni dakika 90 pekee zimetenganisha Bradford na fainali ya kombe hilo la ligi mwaka huu, lakini baada ya kuiondoa Arsenal kwenye kinyanganyiro hicho, mashabiki wengi wanahisi kuwa huenda timu hii inayoshiriki ligi ya chini, ikawashangaza wengi na kuibuka na ushindi.
Ikiwa itafuzi kwa fainali hizo, Bradford itakuwa imeandikisha historia ya kuwa timu ya kwanza tangu mwaka wa 1962, kwa timu inayoshiriki ligi daraja la pili kufika fainali.
Mwaka huo timu ya Rochdale ilifuzu kwa fainali kinyume na matarajio ya wengi.
Post a Comment
0 comments