0

    Na Shomari Binda
         Musoma,

Diwani wa kata ya Mugango katika Wilaya ya Butiama Wandwi Ndaro Kunju (CCM) pamoja na watu wengine watatu wamefikishwa Mahakamani kutokana na tuhuma za mauaji ya ukatili yaliyokuwa yakitokea katika Wilaya za Butiama na Musoma mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha hofu kwa Wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mkoa wa mara imeelezwa na Mwendesha mashitaka Jonas Kaijage mnamo tarehe 21 mwezi wa 12 katika Kijiji cha Kwibara Wilaya ya Butiama washitakiwa wanadaiwa kushiriki katika mauaji ya Tabu Makanya (68) aliyeuwawa na wauaji kukimbia na kichwa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Faisal Kahamba amesema watu hao wametendea kosa hilo kinyume cha kifungu cha 196 na 197 ya kanuni ya adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

Mahamba alisema washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Ndaro Sumuni,Msiba Maregeri na Abeid Kazimiri ambao wote kwa pamoja wanatuhumiwa kushiriki katika tukio hilo la mauaji ya Tabu Makanya.

Kukamatwa kwa Diwani huyo pamoja na watu wengine 15 kutokana na tuhuma mbalimbali za mauaji zimekuja baada ya kuendeshwa kwa oparesheni kubwa inayoongozwa na Mkuu wa kitengo cha Oparesheni kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Saimon Siro pamoja na makachero wengine wa Jeshi hilo kutokana na mauaji mbalimbali yaliyokuwa yakitokea.

Katika tukio la kuuwawa kwa Tabu Makanya ambalo Blog hii ilifatilia mkasa mzima inadaiwa wauaji walivamia nyumbani kwa Marehemu akiwa amelala na watoto wake na kumpiga kisha kuchinjwa kichwa na kuondoka nacho kutokana na kile kilichoelezwa ni imani za kishirikina.

Diwani huyo pamoja na watuhumiwa wengine watatu wa kesi hiyo wamerudishwa rumande huku kesi hiyo ikipangwa kutajwa tena januari 28 mwaka huu.

Post a Comment