0
Na Shomari Binda 
       Musoma,

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome amewafagilia Madiwani wa Halimashauri ya Wilaya ya Musoma ambao wegi wao wanatokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia maslahi ya Umma ikiwemo mahindi ya chakula cha bei nafuu yaliyotolewa na Serikali.

Msome alitoa kauli hiyo alipokuwa akihitimisha juma la kisomo la elimu ya watu wazima katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare na kusema kitendo cha uwajibikaji katika shughuli za kimaendeleo zinapaswa kuungwa mkono.

Alisema katika kufatilia chakula cha bei nafuu kilichotolewa na Serikali katika kukabiliana na njaa Madiwani hao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Manispaa ya Musoma ambayo imedaiwa kuwa na njaa kubwa inapata chakula cha kutosha.

Msome alisema Madiwani wote wamekuwa kitu kimoja katika kulifatilia suala hilo na kuhakikisha Manispaa ya Musoma inapata tani 400 kati ya 900 za mahindi zilizotolewa na Serikali kutoka ghala la Taifa la kuhifadhi chakula Mkoani Shinyanga kuja Mara katika kukabiliana na uhaba wa chakula.

“Katika suala hili Madiwani wameweka itikadi zao pembeni za kisiasa na kushiliki kikamilifu katika kuhakikisha mahindi ya chakula kilichotolewa na Serikali knafika kwa wakati na Wananchi wanapata kutokana na bei elekezi iliyotolewa na Serikali,”alisema Msome.

Alisema tayari mahindi ya chakula katika kukabiliana na njaa yameanza kuingizwa katika Manispaa ya Musoma kutoka kwa wafanyabiashara walioteuliwa na kuuzwa kwa bei elekezi ya Serikali ambapo kilo moja ya mahindi inauzwa kwa bei ya shilingi 700 huku kilo moja ya unga wa sembe ikiuzwa kwa shilingi 900.

Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka Madiwani wa Manispaa ya Musoma kuendelea kutoa ushirikiano katika kufatilia uuzwaji wa mahindi hayo ili Wananchi wasije kuuziwa kwa bei zaidi kutoka kwa wafanyabiashara ambao wameteuliwa.

“Kunaweza kutokea wafanyabiahara wasio waaminifu ambao wanaweza kuwauzia Wananchi mahindi haya kwa bei ya juu naomba tuwe kitu kimoja katika kilifatilia hili ili bei halisi iliyopangwa iweze kutumika katika kuyauza,alisema Msome.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka pia Wananchi kutoa ushirikiano kwa viongozi pale watakapoona wafanyabiashara wanauza mahindi hayo kwa bei ya juu ili waweze kuchukuliwa hatua kutokana na bei hiyo kupangwa na wafanyabiashara walioteuliwa kukubaliana kufata katika ghala la Taifa la kuhifadhi chakula na kuuza kwa bei elekezi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Buhare Lucas Katikilo (CHADEMA) ambaye alikuwa pamoja na Mkuu huyo wa Wilaya katika hitimisho la juma la kisomo alisema watazingatia wito wa Mkuu wa Wilaya katika kufatilia uuzwaji wa mahindi hayo kwa bei elekezi iliyopangwa na Serikali.

Post a Comment