0
MWANAMKE ALIYEHUKUMIWA KIFO NCHINI INDONESIA BAADA YA KUKUTWA NA COCAINE
Mwanamke raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 56, amehukumiwa kifo nchini Indonesia kwa kosa la ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Lindsay Sandiford alikamatwa mwezi Mei mwaka jana baada ya polisi mjini Bali waliokuwa wanafanya ukaguzi wa mizigo kupata kilo 4.8 za cocaine katika mzigo wake.
Sandiford, ambaye anwani yake nchini Uingereza ni Gloucestershire, alisema kuwa alilazimishwa kubeba mzigo huo kuuleta kisiwani Bali.

Wakili wake alisema kuwa waligutushwa na hukumu iliyotolewa na kwamba watakata rufaa.

Sandiford alikamatwa akiwa safarini kutoka Bangkok kuelekea Thailand.

Palikuwa na mshangao mkubwa katika mahakama wakati hukumu ilipotolewa.

Ingawa adhabu ya ulanguzi wa madawa ya kulevya nchini Indoesia ni hukumu ya kunyongwa, upande wa mashtaka ulikuwa umeomba apewe miaka kumi na tano gerezani wakisema kuwa umri wake unapaswa kuwa kigezo cha hukumu ambayo ingetolewa na kwamba hakuwahi kuhusishwa na kashfa zengine.

Lakini wakitoa hukumu hiyo, majaji walisema kuwa utetezi wao haukuwashawishi kuweza kupunguza hukumu hiyo.

Waliongeza kuwa Bi Sandiford hakuonekana kujali kuhusu athari za kitendo chake.

Akiondoka mahakamani, mama huyo kutoka Gloucestershire alionekana kupigwa na mshangao , akifunika uso wake kwa kitambaa.

Wakili wake alisema lazima atakata rufaa na kuongeza kuwa ni nadra kwa majaji kutoa hukumu kama hiyo kinyume na adhabu iliyokuwa imependekezwa na upande wa mashtaka.

Majaji hata hivyo walisisitiza kuwa Sandiford ameharibu sifa ya Bali kama mji wa kitalii na kuhujumu sheria ya serikali dhidi ya madawa ya kulevya.

Bi Sandiford anatuhumiwa kuwa mmoja wa genge la waingereza watatu wanaohusika na ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Post a Comment